NA MWANDISHI WETU
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imewataka Wamiliki wa Mabasi kuhakikisha madereva, Utingo na wahudumu wao wanafuata sheria ambazo zimewekwa na Serikali za kupokea na kusafirisha mizigo.
Imeelezwa sheria hizo zitasaidia kuzuia matumizi ya vyombo hivyo kusafirisha dawa za kulevya na kusisitizwa kwamba kila kifurushi kinapaswa kutambulika mmiliki wake na kuwepo taarifa sahihi za mtumaji na mpokeaji.
Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, amebainisha hayo, leo Juni 12, 2026 katika Kituo Kikuu Cha Mabasi Magufuli (Magufuli Terminal), Mbezi jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa filamu iliyotayarishwa kwa lengo la kutoa elimu kwa umma kuhusu athari za biashara na matumizi ya dawa za kulevya.
"Hatua hiyo itasaidia kubaini wahusika endapo mzigo haramu utagundulika na kuondoa uwezekano wa kuwahusisha watu wasiohusika na uhalifu huo.
Ameongeza kwamba kubeba vifurushi visivyojulikana kunaweza kusababisha madhara ya kisheria kwa dereva, Utingo, wahudumu pamoja na mmiliki wa chombo cha usafiri husika.
Kamishna Jenerali Lymo, katika uzinduzi wa filamu hiyo inayoitwa, Kifurushi ametoa wito kwa wamiliki wa mabasi kuhakikisha zinaoneshwa kwenye mabasi yao ili elimu iendelee kupatikana kwa wadau wote.
Naye Mwenyekiti wa Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA), Abdullah Mohamed, amesema wako pamoja na DCEA katika mchakato wa kutoa elimu kwa wadau ili kudhibiti usafirishaji wa dawa hizo.
Pia Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu LATRA, Halima Lutavi aliipongeza DCEA kwa kufikisha elimu kwa njia ya sanaa.
"Napenda kuwapongeza waandaaji wa filamu na DCEA kwa ubunifu na jitihada zenu za kutumia sanaa kama chombo cha kuelimisha jamii njia yenye nguvu ya kufikisha ujumbe kwa wananchi.
Ambao uleta mabadiliko ya tabia ya jamii yetu, usafirishaji wa madawa ya kulevya ni moja ya changamoto zinazoathiri usalama afya na maendeleo ya taifa letu.
Hivyo uhalifu ama wabebaji kama wasambazaji wa madawa haya wamekuwa wakitumia njia mbalimbali za kusafirisha madawa hayo ambayo pia vyombo vya usafiri, nasi tunaendelea kujipanga Kwa Sheria Kali ili kudhibiti hili", amesema.






No comments:
Post a Comment