NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mashindano ya kuhifadhi Quran yatakayofanyika Chuo Cha Ualimu Vikindu, mkoani Pwani, Machi 14, mwaka huu.
Mashindano hayo ya ngazi ya Kata yanafanyika kwa mara ya nane mwaka huu, huku wito ukitolewa kwa wadau mbalimbali kujitokeza kudhamini shughuli hiyo ili kuleta tija stahiki kwa jamii.
Sheikh Mkuu wa Kata ya Vikindu, Salim Dimoso, amebainisha hayo leo wakati akizungumza kwa njia ya simu na mwandishi wa habari hizi, ambapo amefafanua kwamba lengo la mashindano hayo ni kuhamasisha uhifadhi wa Quran kwa watoto wa kike na wa kiume ndani ya Kata hiyo na mkoa mzima kwa ujumla.
"Mashindano haya yatashindanisha uhifadhi wa Juzuu moja hadi 20, na washiriki watakuwa watoto wapatao 46, wa kike wakiwa 16," amesema Dimoso.
Dimoso amesisitiza kuwa, ili kufikia malengo ya kupata wasomi wazuri na wahifadhi Quran bora, ni vema wadau wakaendelea kujitokeza kudhamini mashindano hayo pamoja na kuwekeza kwa walimu wa dini.
Amesema, masuala hayo ni mambo ya Mungu, hivyo wadau wajikite kudhamini mashindano na kuwekeza kwa walimu wa dini ili kustawisha michakato hiyo na kuifanya kufikia malengo zaidi.
Kwa mujibu wa Sheikh Dimoso, wageni wengine waalikwa wanaotarajiwa kufika katika mashindano hayo, ni pamoja Diwani wa Kata hiyo, Mohamed Maundu na mbunge wa Viti Maalum, Tatu Said.





No comments:
Post a Comment