NA MAGENDELA MRISHO
TAASISI ya Green Mining Awareness imewaita wadau wa sekta ya madini nchini kujadili changamoto zinazowakabili na kupata elimu ya uchimbaji unaozingatia kulinda mazingira.
John Paul, Meneja wa Matukio wa taasisi hiyo, amebainisha hayo leo Aprili 2, 2026 jijini Dar es Salaam na kufafanua kwamba wadau hao wakutana Aprili 17 mwaka huu, Chunya mkoani Mbeya.
"Siku hiyo tutawaeleza umuhimu wa kutumia teknolojia salama, kufuata sheria, kuwa na leseni pamoja na kuepuka kutumia mbinu zisizo salama ikiwemo za kishirikina katika uchimbaji madini," amesema.
Aidha ameongeza kwamba wanaishukuru Serikali pamoja na Wizara ya Madini chini ya Waziri Mavunde kwa kuweka mazingira wezeshi katika sekta hiyo.
Ameongeza kuwa taasisi za kibenki ikiwemo NMB, kampuni zinazouza na kukopesha vifaa vya uchimbaji madini, RM Kyando, Kaeser Compressor na nyinginezo zitakuwepo ili wachimbaji waweze njia sahihi za kuweza kununua au kukopeshwa ili wafikie ndoto zao katika uchimbaji.
Naye Anna Nyange ambaye ni Balozi wa taasisi hiyo, amedadavua kuwa huo ni mwanzo wa harakati za mabadiliko makubwa katika kujenga sekta ya madini iliyoendelevu na yenye manufaa kwa wote.
"Naamini wadau wengi watajitokeza katika mkutano huo wenye fursa zote za elimu, teknolojia na mitandao ya kibiashara ambapo wachimbaji watakutanishwa na wafanyabishara mbalimbali ili kupata njia sahihi ya kufanikiwa kwenye shughuli zao," amesema.





No comments:
Post a Comment