NA MWANDISHI WETU
WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umewataka wadau na wafanyabiashara wa nyanda za juu kusini hususan katika jiji la Mbeya, kuchangamkia fursa za urasimishaji wa biashara ili kuingia kwenye mfumo rasmi wa kiuchumi unaotambulika kisheria utakaowasaidia kuhimili ushindani wa soko la ndani na kimataifa.
Wito huo umetolewa Mei 22, 2026 na Msaidizi wa Usajili Mkuu kutoka BRELA, Hellen Mhina wakati wa maonyesho ya biashara na uwekezaji ya Mbeya City Expo 2026 yanayoendelea jijini humo huku akieleza kuwa urasimishaji ni nguzo kuu inayomlinda mfanyabiashara na kumpa fursa ya kukua kiushindani.
Akizungumza ushiriki wa BRELA katika maonyesho hayo, Mhina alieleza kuwa huo ni muendelezo wa mkakati wa Wakala kufikisha elimu ya urasimishaji biashara kwa watu wengi ambapo kwa sasa huduma za usajili wa Jina la Biashara, Leseni ya Biashara na Leseni ya Kiwanda zinapatika kwenye mfumo ulioboreshwa wa BRELA Online Services (BOS) ambao ni rahisi zaidi kuutumia.
“Kwenye maonesho haya, wananchi wanapata fursa ya kuelekezwa jinsi ya kutumia mfumo huo wa kidijitali wa BOS (BRELA Online Services) ulioanza kutumika hivi karibuni, mfumo huu unarahisisha uwasilishaji wa maombi mapya ya usajili wa majina ya biashara (Business Names) na leseni za viwanda (Industrial Licenses) kwa njia ya haraka na salama zaidi,” alisema Bi. Mhina.
Nao baadhi wafanyabisahara waliotembelea banda la BRELA waliipongeza Wakala kwa kuboresha huduma kupitia mifumo ya usajili na kusogeza huduma hizo katika maonyesho ya Mbeya CIty Expo 2026 wakisema imewasaidia kupata usaidizidi wa kutatua changamoto walizokutana nazo kwenye kusajili biashara na imewapunguzia gharama.
"Nilikuwa na hofu kwamba usajili wa jina langu la biashara ungechukua muda mrefu, lakini nimefika hapa bandani na wataalamu wamenielekeza jinsi ya kutumia huu mfumo wa BOS, ni rahisi sana kuutumia na nimefanikiwa kuondoka na cheti changu hapa hapa uwanjani, imenipunguzia pia gharama za kusafiri,” alisema Bw. Jafari Madunda.
Kwa upande wake ,Asha Mwasanyila ambaye ni mjasiriamali wa usindikaji wa vyakula, alisema elimu aliyopata kwenye banda la BRELA ni muhimu kwake na itamsaidia kuanza mchakato wa kulinda alama yake ya biashara pamoja na kusajili jina lake la Biashara kabla ya kuhitimishwa kwa maonyesho hayo.
Maonyesho ya biashara na uwekezaji ya Mbeya City Expo 2026 yanafanyika kwa siku 10 kuanzia leo Mei 22 na kutamatishwa Mei 31 2026 na BRELA imesogeza huduma zake kwenye maonyesho hayo ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hatua ambayo inaongeza tija kwenye uchumi wa nchi kwani kurasimisha biashara huongeza wigo wa kodi na kuchochea ukuaji wa mapato ya serikali na kuwezesha uboreshaji wa huduma za kijamii nchini.





No comments:
Post a Comment