NAIBU Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ( OWM – TAMISEMI), Sospeter Mtwale, amesema Serikali imejipanga kuhakikisha biashara ya kaboni nchini inatekelezwa kwa uwazi, uwajibikaji na ushirikishwaji wa jamii ili kuwanufaisha wananchi na Taifa kwa ujumla.
Amesema hayo katika Kikao cha Makatibu Wakuu cha kupokea taarifa ya makubaliano ya uendeshaji wa biashara ya kaboni kilichofanyika tarehe 22 Mei 2026 katika ukumbi wa Best Western. Kikao hiki ni utekelezaji wa maagizo ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoyatoa wakati wa ufunguzi wa mkutano wa ALAT jijini Dodoma mwaka 2025, ambapo alielekeza kuwa wadau muhimu washirikishwe kabla ya Halmashauri kusaini mikataba ya biashara ya kaboni ili kuwepo uelewa wa pamoja.
“Serikali inatarajia mikataba yote ya biashara ya kaboni izingatie sheria, kanuni na taratibu pamoja na kuhakikisha uhifadhi wa mazingira unaenda sambamba na maendeleo ya wananchi,” amesema Mtwale.
Mtwale amesisitiza umuhimu wa kuwepo kwa mifumo madhubuti ya ufuatiliaji ili biashara hiyo iwe na tija kwa jamii na Taifa.
Katika kikao hicho, wataalam wamejadili makubaliano yanayotarajiwa kufanywa kati ya Halmashauri za Uvinza na Tanganyika pamoja na kampuni ya Carbon Tanzania Limited kwa ajili ya biashara ya kaboni katika misitu ya Masito, Tongwe Mashariki na Tongwe Magharibi yenye zaidi ya hekta 683,000.
Katika utekelezaji wa maagizo hayo, wizara na taasisi mbalimbali zimeshiriki, zikiwemo Ofisi ya Makamu wa Rais – Mazingira, Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI Wizara ya Fedha, Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji na Tathmini ya Kaboni, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wizara ya Maliasili na Utalii, uongozi kutoka mikoa ya Katavi na Kigoma pamoja na wadau wengine muhimu.











No comments:
Post a Comment