UONGOZI wa Shule ya Awali na Msingi ya Courage iliyoko Kibamba, mkoani Pwani umekabidhi msaada wa chakula, mavazi na bidhaa kwa Kituo cha Watoto Yatima cha Lord’s Children Home kilichoko Kimanzichana wilayani humo.
Msaada huo umekabidhiwa na Meneja wa Shule hiyo, Theodosia Tarimo na kusema msaada huo ni sehemu ya utaratibu wa shule yake, kusaidia jamii hasa zisizojiweza.
“Uongozi, wafanyakazi na wanafunzi tumekuja hapa leo, kutoa tabasamu kwa watoto hawa yatima na wenye mahitaji maalumu,” alisema Theodosia.
Alisema wameamua kwenda kituoni hapo kusaidia watoto hao ambao ni taifa la kesho, na kuchangia malezi na kutimiza ndoto zao.
Theodosia alisema watoto hao kuishi hapo si kwa sababu walimkosea Mungu, bali ni mipango yake katika kuwafikisha kwenye hatima ya maisha yao, hivyo wasichukuliwe kama wakosaji, bali ni sehemu ya makuzi.
“Tunaamini mavazi haya na chakula, vitasaidia kipindi hiki ambacho kituo kina upungufu wa chakula na shule yetu itakuja mara kwa mara kutoa tabasamu kwa watoto,” alisema.
Aliasa wanafunzi wa kituo hicho, kuheshimu viongozi na walezi wao kipindi chote na kujiepusha na makundi maovu ya mtaani yasiyofaa.
Mkurugenzi wa Kituo hicho, Ezekiel Mabesa mbali na kushukuru uongozi wa Shule, aliomba taasisi na mashirika kuiga mfano wa Courage.
“Kama shule tunajua ratiba yenu ni ngumu sana, hata kupata nafasi ya kufanya jambo la kijamii nje ya shule, lakini kwa upendo na uthubutu wenu mmefanya hivyo,” alisema Mabesa.
Alisema kituo kina watoto 33 wa kike na kiume, wenye umri wa kati ya miaka miwili na 16, na wanapa mahitaji yote ya msingi kama watoto wengine wanavyostahili.
“Tunaomba shule nyingine zije kutembelea watoto wetu hapa kituoni na kuwapa faraja," alisema na kuongeza kuwa msaada umekuja wakati mwafaka.
.jpg)




No comments:
Post a Comment