SERIKALI YAAHIDI KUIMARISHA USTAWI WA MABAHARIA, KUKUZA UCHUMI WA BLUU - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Tuesday, June 23, 2026

SERIKALI YAAHIDI KUIMARISHA USTAWI WA MABAHARIA, KUKUZA UCHUMI WA BLUU

 


Katibu Mkuu wa Wizara Ujenzi na Uchukuzi  Zanzibar Mhandisi Ali Said Bakar akizungumza katika Ufunguzi wa  Maadhimisho ya 16 ya Siku ya Mabaharia Duniani mkoani  Kigoma.


NA MWANDISHI WETU

Serikali imesema itaendelea kuchukua hatua madhubuti za kisera na kiutendaji ili kuboresha ustawi wa mabaharia nchini, ikiwa ni pamoja na kulinda haki zao za ajira, kuboresha mazingira ya kazi na kuhakikisha wanapata stahiki zao kwa wakati, kwa kutambua mchango wao mkubwa katika kukuza uchumi wa bluu na maendeleo ya taifa.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhandisi Ali Said Bakar, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, wakati wa ufunguzi wa Maadhimisho ya 16 ya Siku ya Mabaharia Duniani yaliyofanyika mkoani Kigoma.


Mhandisi Bakar alisema mabaharia ni mhimili muhimu wa sekta ya usafirishaji wa majini na maendeleo ya uchumi wa taifa, hivyo changamoto zinazowakabili zinapaswa kushughulikiwa kwa haraka na kwa ufumbuzi wa kudumu.


Alibainisha kuwa Serikali inatambua uwepo wa changamoto mbalimbali zinazowakumba mabaharia, zikiwemo unyanyasaji kazini, ucheleweshaji wa mishahara, ujira usioridhisha pamoja na ukosefu wa huduma muhimu kama bima na matibabu.


 Alisisitiza kuwa hali hiyo inahitaji usimamizi makini kutoka kwa mamlaka husika ili kuhakikisha haki za mabaharia zinalindwa.



“Maadhimisho haya yanatupa nafasi ya kutafakari mchango mkubwa wa mabaharia katika maendeleo ya nchi na kuonesha dhamira ya Serikali ya kushughulikia changamoto zao kupitia sera, sheria na hatua za vitendo,” alisema Mhandisi Bakar.



Aidha, aliwataka wadau na taasisi zote zinazosimamia sekta ya usafirishaji wa majini kuhakikisha zinakuwa mstari wa mbele kusimamia haki za mabaharia, ikiwemo upatikanaji wa bima, huduma za afya na mazingira salama ya kazi.


Akizungumza katika maadhimisho hayo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Hassan Rugwa, alisema kufanyika kwa maadhimisho hayo mkoani humo ni ishara ya kutambua mchango mkubwa wa Kigoma katika usafirishaji wa majini na maendeleo ya uchumi wa bluu nchini.


Alisema maboresho makubwa yaliyotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika miundombinu ya usafiri wa majini yameongeza kwa kiasi kikubwa usafirishaji wa mizigo kupitia njia za maji na kuchochea shughuli za kiuchumi.



“Zaidi ya asilimia 70 ya mizigo katika Mkoa wa Kigoma husafirishwa kwa njia ya maji. Hii inaonesha nafasi kubwa ya mabaharia katika kuimarisha uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla,” alisema Rugwa.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Bahari Zanzibar (ZMA), Fatma Said Sandali, alisema ZMA kwa kushirikiana na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) itaendelea kuimarisha mifumo ya uratibu na usimamizi ili kutatua changamoto zinazowakabili mabaharia na kuboresha mazingira ya kazi katika sekta hiyo.


Aliongeza kuwa maadhimisho hayo pia ni fursa ya kuenzi mchango wa mabaharia waliopoteza maisha wakiwa kazini pamoja na kuonesha mshikamano kwa familia zao.

Sandali alisema katika kipindi chote cha maadhimisho, wananchi watapatiwa elimu kuhusu taaluma ya ubaharia, fursa zilizopo katika sekta ya usafirishaji wa baharini na maziwa, pamoja na umuhimu wa kuzingatia misingi ya kazi yenye utu, usalama na weledi.

Aliwataka mabaharia kuendelea kuzingatia nidhamu, uzalendo na taaluma katika utekelezaji wa majukumu yao, akisisitiza kuwa dunia ya sasa inahitaji wataalamu wa ubaharia wenye ujuzi wa kisasa na viwango vya kimataifa.


Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TASAC, Nahodha Mussa Mandia, alisema mabaharia ni nguzo muhimu ya sekta ya usafirishaji duniani na wanapaswa kupewa kipaumbele katika mipango ya maendeleo ya taifa.


Mandia alisema Serikali imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya usafirishaji wa majini, ikiwemo ujenzi wa Bandari ya Kisasa ya Kalema mkoani Katavi, mradi unaotarajiwa kuongeza biashara, kurahisisha usafirishaji na kuchochea ukuaji wa uchumi wa bluu nchini.


Alisisitiza kuwa pamoja na kutambua mchango wa mabaharia, ni muhimu kwao kuendelea kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za kazi ili kuongeza tija, usalama na ushindani wa sekta ya usafirishaji wa majini.


Maadhimisho ya Siku ya Mabaharia Duniani mwaka huu yanatarajiwa kuhusisha utoaji wa elimu katika mialo ya uvuvi, shule na maeneo mbalimbali ya jamii kwa lengo la kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu mchango wa mabaharia katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania.

Katibu Mkuu wa Wizara Ujenzi na Uchukuzi  Zanzibar Mhandisi Ali Said Bakar akipokea zawadi kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya TASAC Nah.Mussa Mandia mara baada ya  kufungua wa  Maadhimisho ya 16 ya Siku ya Mabaharia Duniani mkoani  Kigoma .









No comments:

Post a Comment