FURAHIKA YAANZISHA KOZI UHUDUMU WA NDEGE, USIMAMIZI MIZIGO - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Monday, July 20, 2026

FURAHIKA YAANZISHA KOZI UHUDUMU WA NDEGE, USIMAMIZI MIZIGO


NA MWANDISHI WETU


 KAIMU Mkuu wa Chuo cha Ufundi Stadi Furahika, Dkt. David Msuya, ametangaza kuanzishwa kwa kozi mpya zinazolenga sekta ya usafiri wa anga (ndege)pamoja na ukaguzi wa mizigo ya treni na kwenye meli ikiwa ni sehemu ya kupanua fursa za mafunzo ya ufundi kwa vijana nchini.



Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Julai 20, 2026, Dkt. Msuya alisema kozi hizo mpya zinahusisha masuala ya usafiri wa anga pamoja na ukaguzi wa mizigo katika treni na meli, ambazo hazikuwa zikitolewa hapo awali chuoni humo.



Alisema Watanzania kutoka mikoa yote wanakaribishwa kujiunga na chuo hicho kwa kutuma maombi kupitia tovuti ya chuo, ambapo wataweza kupata fomu za kujiunga na kufuata taratibu zote za udahili. "Kozi hizi ni mpya kabisa katika chuo chetu, hivyo tunawahimiza vijana kutumia fursa hii kujiunga na kujipatia ujuzi unaohitajika katika soko la ajira," alisema Dkt. Msuya.



Aidha, alibainisha kuwa chuo hicho pia kinatoa mafunzo ya ualimu wa malezi ya watoto (Day Care na Nursery Teaching), huku akieleza kuwa kwa mujibu wa mtaala mpya wa Serikali, kozi hiyo sasa itachukua miaka miwili badala ya mwaka mmoja kama ilivyokuwa awali.



Dkt. Msuya alisema dirisha la udahili wa wanafunzi wapya limefunguliwa na litafungwa Agosti 20, 2026, akiwataka vijana kuwasilisha maombi yao mapema ili kunufaika na nafasi zilizopo.



Alieleza kuwa mbali na kutoa elimu ya ufundi, chuo hicho huwasaidia wanafunzi kupata maeneo ya mafunzo kwa vitendo (field), kuwatafutia ajira na kuwaandalia mazingira bora ya kujifunzia.


 Aliongeza kuwa mafunzo hayo yanatolewa bila malipo ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuwawezesha vijana kujiajiri na kuajirika.



Mbali na kozi hizo mpya, chuo hicho pia kinatoa mafunzo ya lugha za Kichina, Kihindi na Kifaransa kuanzia saa 11 jioni hadi saa 2 usiku, pamoja na kozi nyingine za Hotel Management, Udereva, Uhazili (Secretarial Studies), Kompyuta na fani mbalimbali za ufundi zinazolenga kuongeza ujuzi na ushindani wa wahitimu katika soko la ajira.

No comments:

Post a Comment