MHANDISI MATIVILA AHIMIZA USHIRIKIANO UTEKELEZAJI WA KAZI ZA TARURA - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Saturday, July 25, 2026

MHANDISI MATIVILA AHIMIZA USHIRIKIANO UTEKELEZAJI WA KAZI ZA TARURA


NA MWANDISHI WETU, DODOMA

NAIBU Katibu Mkuu OWM-TAMISEMI anayeshughulikia Miundombinu Mhandisi Rogatus Mativila amewataka viongozi wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kuimarisha ushirikiano na wadau wote ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora ya miundombinu ya barabara inayokidhi matarajio yao.


Mhandisi Mativila ametoa wito huo jijini Dodoma wakati akifunga kikao kazi cha siku nne kilichowakutanisha Menejimenti pamoja na Mameneja wa Mikoa wa TARURA kilicholenga kutathmini utekelezaji wa shughuli za mwaka wa fedha 2025/2026.


Akizungumza wakati wa kufunga kikao hicho amesema barabara zilizo chini ya usimamizi wa TARURA zina nafasi kubwa katika kukuza uchumi wa Taifa kwa kuunganisha vijiji, wilaya na mikoa, hivyo zinapaswa kuendelea kujengwa na kutunzwa kwa viwango vinavyowezesha kupitika katika misimu yote ya mwaka.


"Barabara hizi ni kichocheo muhimu cha maendeleo vijijini na mijini. Tunapaswa kuendelea kuunganisha maeneo yote kwa mtandao wa barabara imara utakaorahisisha usafiri na usafirishaji wakati wote," alisema Mhandisi Mativila.


Aidha, aliwakumbusha viongozi wa TARURA kuwa utekelezaji wa majukumu yao unachangia moja kwa moja kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 pamoja na kuinua ustawi wa wananchi kupitia miundombinu bora.


Katika kusisitiza umuhimu wa ushirikiano Mhandisi Mativila aliwataka Mameneja wa Mikoa kushirikiana kwa karibu na wakurugenzi wa Halmashauri, viongozi wa kisiasa, wananchi na wadau wengine wa sekta ya barabara, akieleza kuwa ushirikiano huo ni msingi wa mafanikio ya Wakala.


Alisema wananchi kwa sasa wana imani kubwa na TARURA kutokana na mchango wake katika kuboresha barabara za vijijini na mijini, jambo linaloongeza matarajio yao ya kuona huduma za miundombinu zinaendelea kuimarika.


"Ni muhimu kutoa nafasi kwa wadau kushauri na kushiriki katika utekelezaji wa miradi. Ushirikiano ndio utakaotuwezesha kufikia malengo ya Wakala na kuwahudumia wananchi kwa ufanisi zaidi," alisisitiza.


Katika kikao kazi hicho, jumla ya mawasilisho 18 yaliwasilishwa yakihusu masuala mbalimbali ya maendeleo ya Wakala, ikiwemo taarifa ya fedha, Mpango Endelevu wa Usimamizi wa hifadhi ya Barabara za TARURA 2025, matumizi ya Mfumo wa DROMAS, mpango wa mafunzo kwa watumishi, utekelezaji wa Kanuni za Maadili katika Utumishi wa Umma, mfumo wa e-Mrejesho, maendeleo ya miradi ya CERC pamoja na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.





No comments:

Post a Comment