Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetabiri mvua za msimu wa Vuli wa Oktoba hadi Desemba 2026 kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mbalimbali nchini, huku ikiwataka wananchi na wadau kuchukua tahadhari mapema kutokana na uwezekano wa vipindi vya mvua kubwa na mafuriko.
Kwa mujibu wa TMA, mvua hizo zinatarajiwa kuanza katika wiki ya kwanza na ya pili ya Oktoba katika maeneo ya Arusha na Manyara, pamoja na ukanda wa Kaskazini unaojumuisha Tanga, Dar es Salaam, kaskazini mwa Morogoro, Mafia na Pemba.
“Wananchi wanapaswa kufuatilia taarifa rasmi za hali ya hewa na kuchukua hatua mapema ili kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na mvua kubwa,” TMA imesema.
MAFURIKO NA KILIMO
TMA imeonya kuwa mvua nyingi zinaweza kuongeza unyevunyevu wa udongo na kusababisha mafuriko, hali inayoweza kuathiri shughuli za kilimo na uzalishaji wa chakula.
Pamoja na changamoto hizo, mvua zinaweza kuongeza uzalishaji katika maeneo yatakayotumia vizuri fursa hiyo. Wakulima wametakiwa kuandaa mashamba, kupanda kwa wakati, kutumia pembejeo sahihi na kuboresha usimamizi wa maji.
“Wakulima wanashauriwa kutumia mbinu bora za kilimo, kuvuna maji ya mvua na kuchukua hatua za kudhibiti visumbufu vya mimea ili kupunguza athari na kuongeza uzalishaji,” imesema TMA.
BARABARA, MADARAJA NA USAFIRI
Mamlaka hiyo imeonya kuwa mvua kubwa zinaweza kusababisha mafuriko, mmomonyoko wa udongo, kuharibika kwa barabara na madaraja, hali inayoweza kuvuruga usafiri na kuongeza hatari ya ajali.
Bandari nazo zinaweza kukumbwa na mawimbi makubwa na hali mbaya ya bahari, huku usafiri wa anga ukiathiriwa na mwonekano hafifu na kuchelewa kwa safari.
TMA imewataka wadau wa usafiri kukagua miundombinu mara kwa mara na kufuatilia taarifa za hali ya hewa ili kuchukua hatua kwa wakati.
AFYA NA MAZINGIRA
TMA pia imeonya kuhusu uwezekano wa kuongezeka kwa magonjwa kutokana na maji kutuama, kuathirika kwa mifumo ya maji taka na uchafuzi wa vyanzo vya maji.
Mamlaka za afya zimetakiwa kujiandaa kwa changamoto hizo, huku wananchi wakihimizwa kuchukua hatua za usafi na kuzuia maji kutuama katika maeneo ya makazi.
WAFUGAJI NA WAVUVI
Wafugaji wametakiwa kupanga matumizi ya maji na malisho pamoja na kufuatilia ushauri wa wataalamu wa mifugo.
Wavuvi na wakulima wa mwani nao wametakiwa kufuatilia taarifa za hali ya hewa na bahari kabla ya kuanza shughuli zao ili kupunguza hatari zinazoweza kujitokeza.
SERIKALI ZA MITAA ZATAKIWA KUJIANDAA
TMA imezitaka serikali za mitaa kuimarisha mifumo ya mifereji, kuondoa vizuizi kwenye njia za maji na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kujikinga na mafuriko.
“Maandalizi ya mapema ni muhimu katika kupunguza madhara ya matukio ya hali mbaya ya hewa,” TMA imesisitiza.
TMA imesema pia imeendelea kuboresha utabiri wa hali ya hewa hadi ngazi ya wilaya, hatua inayolenga kuwasaidia wananchi, wakulima, wafugaji, wafanyabiashara na serikali kupanga shughuli zao kwa kuzingatia mwenendo wa hali ya hewa.
Mamlaka hiyo imewataka wananchi kuendelea kufuatilia taarifa za kila siku, angalizo na tahadhari rasmi zitakazotolewa kadiri hali ya hewa itakavyobadilika.
“Taarifa rasmi za hali ya hewa zinapaswa kuwa chanzo cha msingi katika kuhabarisha na kuelimisha jamii kuhusu matukio yanayoweza kujitokeza,” TMA imesema.





No comments:
Post a Comment