PROF. KABUDI AWATAKA WANANCHI KUZINGATIA TAHADHARI ZA MAAFA - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Wednesday, August 19, 2026

PROF. KABUDI AWATAKA WANANCHI KUZINGATIA TAHADHARI ZA MAAFA

 


NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu–Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Prof. Palamagamba Kabudi, amewataka wananchi kuzingatia tahadhari na maelekezo yanayotolewa na wataalamu na mamlaka husika ili kupunguza madhara yanayotokana na majanga na maafa.


Prof. Kabudi ametoa wito huo tarehe 19 Agosti, 2026 wakati akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Watoa Huduma za Misaada ya Kibinadamu Duniani yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.


“Ushiriki wa wananchi ni muhimu katika kuimarisha ustahimilivu wa jamii dhidi ya majanga, huku akiwataka kuendelea kufuata taarifa na maelekezo rasmi kutoka kwa wataalamu na mamlaka zinazohusika na masuala ya maafa.”


Katika hatua nyingine, alisema Serikali itaendelea kuimarisha mifumo ya tahadhari za mapema na kujenga ustahimilivu wa jamii ili kuongeza uwezo wa wananchi kukabiliana na majanga na kupunguza madhara yanayotokana na matukio hayo.


Alisema uwezo wa nchi katika kukabiliana na majanga kwa ufanisi unategemea uwepo wa mifumo madhubuti, uratibu na ushirikiano wa karibu na wenye tija kati ya Serikali na wadau wa huduma za kibinadamu.


Prof. Kabudi pia alimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mchango wake katika kusimamia masuala ya kibinadamu na ustawi wa wananchi.


“Kupitia uongozi wa Rais Dkt. Samia, Serikali imeendelea kuhakikisha wananchi wanaokumbwa na changamoto za majanga wanapata msaada na faraja wakati wa dharura.”


Prof. Kabudi aliwataka watoa huduma za kibinadamu kuwekeza zaidi katika kuwawezesha wananchi kwa elimu na taarifa sahihi kuhusu vihatarishi vinavyowazunguka, pamoja na hatua za kuchukua kabla, wakati na baada ya janga.


Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Dkt. James Kilabuko, amesema maadhimisho ya siku hiyo yanatoa fursa ya kutambua na kuthamini mchango wa watoa huduma za kibinadamu ambao hujitolea kwa moyo wa huruma, ujasiri na mshikamano katika kuokoa maisha na kupunguza madhara.


Alisema ni muhimu kuendelea kuimarisha ushirikiano na mshikamano miongoni mwa Serikali, wadau wa huduma za kibinadamu na jamii katika kuhakikisha kuwa msaada unapatikana kwa wakati na unawafikia wale wanaouhitaji.


“Ni muhimu kuhakikisha kuwa katika kila hatua ya utoaji wa huduma za kibinadamu, maisha, usalama na utu wa mwanadamu vinaendelea kuwa kiini cha hatua tunazochukua.”





No comments:

Post a Comment