BRELA - WAFANYABIASHARA WENGI WANASHINDWA KUPATA MIKOPO KUTOKANA NA KUTOSAJILI BIASHARA ZAO - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Saturday, September 26, 2026

BRELA - WAFANYABIASHARA WENGI WANASHINDWA KUPATA MIKOPO KUTOKANA NA KUTOSAJILI BIASHARA ZAO


NA MWANDISHI WETU, GEITA

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umesema wafanyabiashara wengi wanajikwamisha wenyewe kupata mikopo na zabuni kwa kushindwa kusajili biashara zao.


Akizungumza katika Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Geita, Afisa wa BRELA, Salum Makuka alisema taasisi za fedha na zabuni zote zinamtaka mfanyabiashara awe na usajili halali.


Amesema BRELA imeamua kusogeza huduma zake karibu na wananchi kwenye maonesho hayo, ambapo huduma zote zinatolewa papo hapo bure, isipokuwa ada ya kisheria ya Serikali.



"Tumeleta huduma hizi hapa ili wananchi wapate elimu na pia waweze kusajili biashara zao papo hapo. Urahisishaji wa kupata huduma ni bure," alisema Makuka.


Alizitaja huduma zinazotolewa kuwa ni usajili wa kampuni, majina ya biashara, nembo (trademarks), viwanda vidogo, leseni za Daraja A na hati miliki (patent).


Makuka alionya kuwa kuchelewa kusajili jina la biashara kunaweza kumfanya mfanyabiashara kupoteza jina alilojenga kwa jasho kwa miaka mingi endapo mtu mwingine atatangulia kulisajili.



Alisema BRELA pia inatoa elimu kuhusu mfumo mpya wa kidijitali wa BOS unaomuwezesha mfanyabiashara kufungua akaunti, kusajili biashara, kuwasilisha taarifa za mwaka na kulipa ada za uendelezaji mtandaoni.


Naye mfanyabiashara wa Nayubi Cosmetics aliyenufaika na huduma hiyo alisema alikuwa amesajili jina la biashara mwaka jana bila kujua umuhimu wa nembo, lakini kupitia maonesho ya mwaka huu amepata elimu na kusaidiwa kuongeza usajili.


BRELA itaendelea kutoa huduma hizo hadi Oktoba 3, huku ikiwataka wachimbaji na wajasiriamali kutumia fursa hiyo kujifunza na kulinda biashara zao kisheria.

No comments:

Post a Comment