FDH, STAMICO WAUNGANA KUWAINUA WATU WENYE ULEMAVU - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Saturday, September 26, 2026

FDH, STAMICO WAUNGANA KUWAINUA WATU WENYE ULEMAVU



NA MWANDISHI WETU, GEITA

 Shirika la FDH Tanzania limepongeza ushirikiano wake na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) katika kuwawezesha kiuchumi na kijamii watu wenye ulemavu pamoja na makundi mengine katika jamii.


Akizungumza leo Septemba 26, 2026 kwenye Maonesho ya Tisa ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan mkoani Geita, Mkurugenzi wa FDH Tanzania, Michael Salali amesema ushirikiano huo umewasaidia watu wenye ulemavu kuunganishwa na fursa mbalimbali za kujitegemea.


Salali amezipongeza juhudi za STAMICO chini ya uongozi wa Mkurugenzi wake, Dkt. Venance Mwasse, kwa kutoa kipaumbele kwa makundi ya watu wenye ulemavu.


"Tunawapa elimu na mwongozo wa kutambua fursa kwenye sekta mbalimbali. Huu ndio uwezeshaji wa kweli," alisema Salali.


Katika hatua nyingine, STAMICO imetambulisha bidhaa yake mpya ya nishati safi ya mkaa mbadala uitwao Rafiki Briquette, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala.


Wataalamu wa STAMICO waliopo bandani hapo wako tayari kutoa elimu kwa wananchi kuhusu uzalishaji na matumizi ya nishati hiyo, huku FDH ikiwataka watu wenye ulemavu kutumia fursa hiyo kutembelea banda hilo kupata ushauri.


Salali ametoa wito kwa taasisi na Watanzania kwa ujumla kuendelea kuwawezesha watu wenye ulemavu.


“Watu wenye ulemavu wanahitaji fursa na mazingira wezeshi ili waweze kutumia uwezo wao na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii,” amesema.


Aidha, ameishukuru Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa msisitizo wake wa uwezeshaji wa wananchi na matumizi ya nishati safi.



No comments:

Post a Comment