FEDHA ZA MABADILIKO YA TABIANCHI ZIWAFIKIE WAKULIMA: SIBANDA - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Sunday, September 27, 2026

FEDHA ZA MABADILIKO YA TABIANCHI ZIWAFIKIE WAKULIMA: SIBANDA


NA MWANDISHI WETU

WAKULIMA wadogo wa Afrika Mashariki wamezitaka Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuhakikisha fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zinawafikia wakulima na jamii kwa wakati ili kuwawezesha kukabiliana na athari za mabadiliko hayo.


Wito huo umetolewa katika Jukwaa la Kikanda la Wakulima wa EAC kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, lililofanyika wakati jumuiya hiyo ikiandaa Mkakati na Mpango Kazi wake wa Miaka 10 wa Mabadiliko ya Tabianchi (2026–2036).


Akizungumza katika mdahalo huo uliofanyika kwa njia ya mtandao, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wakulima Wadogo wa Mashariki na Kusini mwa Afrika (ESAFF), Diane Sibanda, alisema mabadiliko ya tabianchi yameshakuwa uhalisia wa kila siku kwa wakulima na yameathiri uzalishaji, kipato, usalama wa chakula na maisha kwa ujumla.


Alisema wakulima wanakabiliwa na mvua zisizotabirika, ukame wa muda mrefu, mafuriko, kupanda kwa joto, wadudu na magonjwa yanayoendelea kuathiri uzalishaji wa kilimo.


Sibanda alisema hatua za kukabiliana na tabianchi zinapaswa kuhakikisha wakulima wadogo na jamii sio tu wanufaika, bali ni washiriki hai katika kuunda, kutekeleza, kufuatilia na kutathmini sera na programu za tabianchi.


“ESAFF inataka ushiriki wa wakulima wadogo uwekwe kisheria, ikiwemo wanawake, vijana na makundi yaliyo hatarini, katika kupanga, kutekeleza, kufuatilia na kutathmini Mkakati na Mpango Kazi wa EAC wa Mabadiliko ya Tabianchi,” alisema.


*Kilimo Ikolojia Kiwe Kiini cha Mkakati*


Sibanda pia ameitaka EAC kuifanya dhana ya kilimo ikolojia (agroecology) kuwa kiini cha kukabiliana na tabianchi kwa kutafsiri ahadi za usimamizi endelevu wa ardhi kuwa vitendo halisi na bajeti mahususi za kusaidia mbinu zinazoongozwa na wakulima.


Kuhusu fedha za tabianchi, ESAFF imetaka kuwe na mifumo rahisi na inayofikika ya kifedha ili kuhakikisha fedha za kukabiliana na tabianchi zinawafikia mashirika ya wakulima na jamii ngazi ya chini.



Aidha, jukwaa hilo limependekeza kuimarisha uwajibikaji wa kijamii unaoongozwa na wakulima kwa kuwawezesha wakulima kufuatilia bajeti za tabianchi, ahadi na utekelezaji kupitia kadi za alama za jamii, ufuatiliaji wa matumizi ya umma na ufuatiliaji shirikishi.


*Kuunganisha na Mifumo ya Kikanda*


Kwa mujibu wa ESAFF, mkakati huo unapaswa kuoanishwa na mifumo ya kikanda na bara, ikiwemo Azimio la Kampala la CAADP na Mpango wa Uwekezaji wa Mifumo ya Chakula ya Kikanda ya EAC (RASIP), ili kuimarisha mshikamano wa sera, utekelezaji na utoaji taarifa.


Mkakati huo pia unapaswa kuunganishwa na Michango ya Kitaifa Iliyoamuliwa (NDCs), Mipango ya Kitaifa ya Kukabiliana na Tabianchi na Mkataba wa Paris, huku ukiimarisha mchango wa Afrika Mashariki katika mijadala ya tabianchi duniani.


Jukwaa hilo la kikanda pia linatarajiwa kuandaa mapendekezo kuelekea Mkutano wa 31 wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP31), ikiwemo wito wa hatua za tabianchi zinazomweka mkulima mdogo katikati ya juhudi za kukabiliana na mabadiliko.


Mapendekezo hayo yanatarajiwa kusisitiza upatikanaji wa moja kwa moja wa fedha za tabianchi kwa wakulima na jamii, uwekezaji katika kilimo ikolojia na mifumo ya mbegu zinazosimamiwa na wakulima, pamoja na kuanzisha mfumo wa Malipo ya Hasara na Uharibifu kwa wakulima walioathirika na mabadiliko ya tabianchi.


Sibanda aliwataka wakulima kushiriki wazi uzoefu, vipaumbele na suluhisho zao, huku akiwataka watunga sera na washirika wa maendeleo kusikiliza na kutafsiri mapendekezo hayo kuwa hatua halisi chini ya Mkakati mpya wa EAC wa Mabadiliko ya Tabianchi.

No comments:

Post a Comment