IDP YACHANGIA UHIFADHI MAZINGIRA - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Thursday, September 17, 2026

IDP YACHANGIA UHIFADHI MAZINGIRA


NA MWANDISHI WETU


MKURUGENZI wa Halmashauri ya Arusha, Suleiman Msumi amepongeza Shirika la Island of Peace (IDP) kupitia Mashirika ya RECODA na Mtandao wa Vikundi vya Wakulima mkoani Arusha (MVIWAARUSHA), kuwezesha upandaji wa miti 50,000 kupitia mradi ya kilimo ikolojia.


Msumi ametoa pongezi hizo Septemba 15, wakati wa hafla ya uzinduzi wa miradi mipya mitatu ya Kilimo Endelevu Arusha+II, ECO-FOOD II na SAFI yenye lengo la kuendeleza kilimo ikolojia na lishe bora, ambayo inatarajiwa kutekelezwa kwa miaka miwili na mitatu kwa gharama ya shilingi bilioni 3.


Amesema kilichofanywa na taasisi hizo kupanda miti 50,000 kwa miaka mitatu ni cha kupongezwa na kuigwa na wadau wote, ili jitihada za serikali kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yameleta madhara kwa nchi na dunia.


Msumi amesema mradi huo umekuwa na mafanikio makubwa katika utunzaji wa rasilimali za udongo na mimea kwa ajili ya kizazi kijacho.


"Kama tunavyofahamu, vyanzo vya maji vinakauka na mvua zinanyesha bila msimu kwa sababu ya ukataji miti ovyo. Mradi huu wa upandaji miti ni mkubwa na wa kipekee, tunapaswa kuunga mkono," amesema.


Amewashauri wakulima walionufaika na mradi huo kutumia ujuzi, rasilimali na fedha walizopata kupanua wigo wa kilimo na kuongeza mnyororo wa thamani.


"Tumeona misingi imewekwa. Twendeni tukatumie elimu hiyo kuwa mabalozi kwa wakulima wengine walikosa fursa. Elimu hiyo isibaki kwenu, ishusheni kwa lugha rahisi. Kesho tukisema mmehitimu, kuwe na thamani kubwa nyuma yenu," amesisitiza.


Kwa upqnde mwingine Mkurugenzi Msumi ametoa raia kwa wakulima na wananchi kufuata maelekezo ya Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), yanayoonesha uwepo wa mvua kunwa za El Niño zinazoambatana na upepo kuanzia mwisho wa mwezi Septemba hadi Desemba.


"Niwaombe tuchukue tahadhari. Mvua hizi ni kali na zina uharibifu mkubwa. Tuimarishe miundombinu ya kuhifadhi maji ili mazao yetu yasibebwe na mafuriko. Tuelimishe wengine kuwa mabalozi wa kuhakikisha mashamba hayaharibiki, tujiwekee na kuhifadhi chakula cha kutosha ili kesho tusiwe na balaa la njaa," ameonya.


Aidha Msumi aliishukuru IDP kuwezesha shule za msingi na sekondari 15 za Halmashauri ya Arusha na Karatu kupata chakula mashuleni, hali ambayo imeongeza ufaulu, mahudhurio na nidhamu kwa wanafunzi.


"Tuna ushuhuda kabisa, kabla ya wanafunzi kula shuleni na baada ya kuanza, ufaulu umepanda. Utoro umekuwa historia kwa baadhi ya shule kwa sababu concentration ya wanafunzi imekuwa kubwa, performance zimeongezeka maradufu na hata tabia zao zimekuwa nzuri. Hii ni sadaka na ni thawabu kubwa," amesema.


Pia ameishukuru IDP kwa kutowaacha njiani na kuamua kuendelea na awamu nyingine ya miaka mitatu hadi 2029, na kuwataka wakulima kutumia fursa hiyo adhimu kwa manufaa ya familia zao na Taifa kwa ujumla, kwa kuzingatia kauli mbiu ya "Afya imara ndio msingi wa maendeleo" na kupitia matumizi ya chakula cha asili kisicho na kemikali.


Mkurugenzi wa IDP, Ayesiga Buberwa amesema wamejipanga kutoa elimu kwa wakulima ya maandalizi ya kukabiliana na El Nino.


"IDP imeanza kuchukua hatua za maandalizi kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na utabiri wa uwepo wa El Niño katika kipindi cha Oktoba, Novemba na Desemba, ikisisitiza umuhimu wa wakulima kupata taarifa sahihi na kujiandaa mapema badala ya kusubiri athari zitokee," amesema.


Ayesiga amesema taarifa za utabiri wa hali ya hewa zinapaswa kuwa kichocheo cha maandalizi na si sababu ya kusubiri tukio litokee.


Amesema IDP, kupitia timu zake za miradi, inapanga kuzunguka vijijini kuwafikia wakulima na kutoa taarifa na elimu kuhusu hatua zinazoweza kuchukuliwa kukabiliana na changamoto zinazoweza kusababishwa na mvua nyingi, ikiwemo usalama wa miundombinu ya maji, pamoja na uhifadhi wa mazao na chakula.


"Tusisubiri El Niño ije ndipo tuanze kuchukua hatua. Tujipange mapema na kuhakikisha wakulima wanapata taarifa sahihi."


Ayesiga amesema maandalizi hayo pia yataangalia namna ya kuhakikisha visima vya umwagiliaji na miundombinu ya maji iko katika hali salama, huku wakulima wakipewa mbinu bora za kuhifadhi mazao ili kupunguza hasara zinazoweza kusababishwa na mvua nyingi.


Ameongeza kuwa changamoto ya mabadiliko ya tabianchi inaweza kutumika kama fursa ya kuonesha uwezo wa mbinu za kilimo ikolojia katika kujenga mifumo ya chakula inayostahimili misukosuko ya tabianchi.







No comments:

Post a Comment