Simba mwaka wao huu! - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Wednesday, October 19, 2011

Simba mwaka wao huu!

- Wavunja daraja la Ruvu, Yanga na ndugu zao leo
- Kocha Toto: Siwezi kufungwa na mwanangu
Na Asha Kigundula
KAMA kawa! Wanaweza kusema hivyo mashabiki wa Simba baada ya timu yao kuifumua Ruvu Shooting kwa mabao 2-0, katika mchezo wa jana wa Ligi Kuu ya Vodacom uliopigwa kwenye Uwanja wa Azam uliopo Chamazi, Dar es Salaam.
Simba ilianza mchezo kwa kasi kama kawaida yake ya kutaka kuendeleza wimbi lake la ushindi ikiwatumia wakali wake Emmanuel Okwi, Patrick Mafisango na Uhuru Selemani.
Lakini pamoja na jitihada kubwa walizofanya, timu hizo zilimaliza kipindi cha kwanza bila kufungana, ingawa zote zilionesha kuhitaji bao bila kuwa na mipango endelevu ya kuwazidi mabeki ujanja.
Abdallah Juma na Kassim Linde walishindwa kufunga pamoja na kuingia mara nyingi katika eneo la hatari la Simba na kufanikiwa kuichanganya kwa muda safu ya ulinzi ya mabingwa hao wa zamani.
Baada ya kutokuwa na mafanikio katika kipindi cha kwanza, kocha wa Simba, Moses Bassena alimtoa Uhuru Seleman na kumuingia Haruna Moshi 'Boban' kwa ajili ya kuongeza mashambulizi.
Mabadiliko hayo yalifanya kazi ndani ya dakika mbili tu, kwani pasi ya Boban ilitumiwa vizuri na Okwi aliyekwamisha mpira wavuni kuipa Simba bao la kuongoza.
Kasi ya Simba iliendelea, na dakika ya 54, Boban aliiandikia Simba bao la pili akimalizia kirahisi pasi ya Okwi huku akikataa kushangilia pamoja na wenzake kumfuata kwa mbwembwe.
Ruvu walishitushwa na mabo hayo na kuanza kujipanga upya, safu yake ya ushambuliaji ilifanikiwa kuamka na kucheza vizuri na Juma Mdindi aliyeingia kuchukua nafasi ya Linde angeweza kuipa timu yake bao, lakini shuti lake makini liligonga nguzo na kurudi uwanjani.
Pamoja na kasi nzuri na mipango ya ushambuliaji ya Ruvu Shooting, walishindwa kupata hata bao moja la kufutia machozi huku Simba nayo ikiridhika na mabao hayo mawili hadi mwisho wa mchezo.
Ushindi huo wa Simba umezidi kuichimbia kileleni timu hiyo ikiwa na pointi 24 sasa kutokana na kupata sare michezo mitatu na kushinda yote iliyocheza msimu huu.
Ligi hiyo inaendelea tena leo kwa mchezo mmoja ambapo mabingwa watetezi, Yanga watakuwa katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuvaana na ndugu zao, Toto African ya Mwanza.
Mabingwa hao wenye makazi yao Mitaa ya Twiga na Jangwani jijini Dar es Salaam wanashika nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 15, baada ya kucheza mechi tisa, ikitoka suruhu mechi tatu na kufungwa mechi mbili.
Akizungumzia mchezo huo wa leo, kocha wa Toto African, John Tegete, alisema ana uhakika wa timu yake kuifunga Yanga pamoja na kuwa katika kiwango kizuri katika michezo ya sasa.
Tegete alisema hawezi kufungwa na timu anayocheza mtoto wake, hivyo pointi tatu za mchezo wa leo zitakuwa halali yao na muhimu kwa ajili ya kurudisha imani ya kuwa mabingwac msimu huu.
"Siwezi kufungwa na timu anayocheza mwanangu, nina uhakika wa pointi tatu za leo ni mali yangu kwa sababu mimi ni mwalimu sitaweza kufungwa na mwanafunzi ambaye nimemfundisha mwenyewe," alisema Tetege.

No comments:

Post a Comment