T-Moto kuanza kuwarusha Mtwara - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Tuesday, October 18, 2011

T-Moto kuanza kuwarusha Mtwara

Na Mwandishi Wetu
KUNDI jipya la taarabu linalokuja kwa kasi nchini, Tanzania Modern Taarab (T-Moto) ama ‘Real Madrid’ linatarajia kuanza kufanya maonesho mawili katika Mkoa wa Mtwara.
Akizungumza na Jambo Leo jana, Mkurugenzi wa T-Moto, Amini Salmini, amesema mara tu baada ya uzinduzi wa kundi hilo unaotarajia kufanyika Oktoba 28 kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam, kundi hilo tayari lina mwaliko wa Oktoba 29 na 30, mkoani Mtwara.
Alisema mara tu baada ya kumaliza onesho la uzinduzi huo, wasanii wataondoka jijini usiku huo huo kuanza safari ya kuelekea Mtwara ambako watafanya maonesho mawili.
Onesho la kwanza la Oktoba 29, linatarajia kufanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Makonde Beach Club, na onesho la pili litafanyika Oktoba 30 Nachingwea.
Pia, Salmini alisema kuwa kabla ya kufanya onyesho la pili wasanii wa kundi hilo watatembelea wagonjwa katika Hospitali ya Mkoa huo husasan wodi ya wazazi na watoto, ambapo watatoa msaada wa kitanda cha kuzalia cha wajawazito katika hospitali hiyo pamoja na kutoa msaada wa vitu mbalimbali kwa watoto waliolazwa katika hospitali hiyo.
Salmini alisema katika uzinduzi wa kundi hilo Bendi ya Mapacha Watatu na Msondo Ngoma, zitakuwa bega kwa bega katika kutoa burudani za kusindikiza kabla ya kupanda jukwaani kwa kundi hilo jipya.
Albam hiyo ya kwanza ya kundi hilo imebebwa na wimbo wa Bi Mwanahawa Ally, uitwao Aliyeniumba Hajanikosea, ambapo pia itakuwa na nyimbo nyingine kali zilizoanza kusikika katika vituo mbalimbali vya redio.
Nyimbo nyingine ni wimbo wa Jokha Kassim, ambao tayari umeshaanza kuzua gumzo miongoni mwa mashabiki wa muziki wa Taarab, ambao hauishi kujadiliwa, uitwao Unavyojidhani Hufanani.
Nyingine zinazokamilisha albam hiyo ni pamoja na Mchimba Kaburi Sasa Zamu yake Imefika ni ‘Dongika, ulioimbwa na Mrisho Rajab, aliyejitosa katika fani ya muziki wa Taarab akitokea katika shindano la BSS, pamoja na Riziki Shotcut, ulioimbwa na Aisha Masanja.

Wanamuziki wa T- Moto wakiwa katika mazoezi makali, aliyesimama ni mwimbaji wa kundi hilo jipya, Hassan Ally akionesha umahiri wa kushusha mistari tayari kwa uzinduzi wake.

No comments:

Post a Comment