Na Eben-Ezery Mende
WASANII wakali katika muziki wa Bongo Fleva, Chegge, Mheshimiwa Temba na Mataluma wamethibitisha kushiriki katika utoaji burudani kwenye tamasha la bendi ya Twanga Pepeta litakalofanyika Novemba 6 mwaka huu.
Tamasha hilo litakalofanyika katika Viwanja vya Leaders Club, Kinondoni ambalo litawahusisha wasanii litakuwa ni maalum pia kwa uzinduzi wa albamu ya 11 ya bendi hiyo iitwayo 'Dunia Daraja', sambamba na sherehe za miaka 50 ya Uhuru wa Tanganyika.
Akizungumza na Jambo Leo Dar es Salaam jana, Mratibu wa tamasha hilo, Hassan Rehani, alisema tamasha hilo pamoja na mambo mengine pia litakuwa maalumu kwa ajili ya watu wote ambao wameiunga mkono bendi hiyo tangu kuanzishwa kwake.
Rehani alisema kuwa pamoja na wasanii hao, pia wapo wasanii wengine ambao ni Isha Mashauzi ambaye atarindima na kundi lake la Mashauzi Classic, Msondo Ngoma 'Baba ya Muziki', Schengen Academy na Prince Dully Sykes 'Mr Misifa'
Kwa kujigamba, Rehani alisema wamo wasanii wengi ambao bado ASET inafanya nao mazungumzo ili wafanye onesho kwenye tamasha hilo.
Alisema sehemu kubwa ya tamasha hilo itahusisha uzinduzi wa albamu ya 11 ya bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta' iliyopewa jina la 'Dunia Daraja'.
| BAADHI YA WASANII WA TWANGA PEPETA |
--------
P Funk abadilisha studio yake
Na Geofrey Nanai
BAADA ya kuwa kimya kwa muda mrefu, ujio mpya wa studio kongwe ya muziki wa kizazi kipya (Bongo Records) umewashitua wadau na wasambazaji wa muziki nchini.
Akizungumza na Jambo Leo Dar es Salaam jana, mmiliki wa studio hiyo, Alfani Majani 'P Funk' alisema ukimya huo ulitokana na vyombo vya kurekodia kuchakaa na kuamua kuvibadilisha na kuagiza vipya kutoka nje ya nchi.
Alisema marekebisho ya studio na mandhali ya nje pia yamechangia kwa kiasi kikubwa kuwa kimya kwa muda sasa bila kusikika kwa kazi zake mpya redioni.
''Nimeamua kuifanyia studio yangu marekebisho ili kuiongezea nguvu na ladha tofauti niweze kukabiliana na ushindani uliopo hivi sasa katika tasnia ya muziki nchini,'' alisema P Funk.
Aidha, alisema pamoja na ukimya huo, tayari amesharekodi baadhi ya nyimbo na kusambazwa katika vituo mbalimbali vya redio na zinafanya vizuri kwani amesha pokea pongezi nyingi kutoka kwa wadau wa muziki nchini.
Aliwataja wasanii wakongwe waliokwisharekodi katika ujio wake mpya kuwan ni pamoja na Juma Nature, Bonta, Fanani wa Hard Blastaz, Jay Mo na Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi 'Sugu'.
Chaneta kupamba sherehe za Uhuru kwa michuano
Na Hamisi Magendela
CHAMA cha Netbali Tanzania (CHANETA) kipo katika maandalizi ya mashindano ya Kombe la Uhuru yanayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Novemba 30 mwaka huu.
Akizungumza na Jambo Leo Dar es Salaam jana, Naibu Katibu Mkuu wa CHANETA, Rose Mkisi, alisema Tanzania itawakilishwa na klabu kutoka Tanzania Bara na Visiwani.
"Katika mashindano hayo pia tumealika klabu kutoka Afrika Mashariki katika nchi za Kenya, Uganda, Burundi pamoja na Rwanda, ambao tunaamini wenzetu watatoa upinzani mkubwa kwetu," alisema Mkisi.
Alisema lengo la mashindano hayo ni kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru wa Tanganyika inayofikia kilele Desemba 9 mwaka huu, sambamba na kuimarisha wachezaji wa hapa nyumbani katika mchezo huo.
Mkisi amezitaka timu shiriki kufanya mazoezi ya kutosha ili kuleta ushindani katika mashindano hayo yanayotarajiwa kumalizika Desemba 8, siku moja kabla ya maadhimisho ya kitaifa.
Mkenya kumjaribu Kamote
Na Asmah Mokiwa
Rais wa Oganaizesheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBO), Yasin Abdallah 'Ustaadh', amesema Novemba 6, bondia machachari kutoka Tanga, Allan Kamote atapambana na Fredrick Nyakesa kutoka Kenya.
Pambano hilo litakuwa la kimataifa la kirafiki litakalofanyika kwenye Ukumbi wa Ridoch mkoani Tanga, likiwa la raundi nane uzito wa kilo 61.2 (Light Weigth).
Alisema kitakuwa pia na mapambano mengine ya utangulizi ambayo yatawakutanisha mabondia kadhaa kutoka Tanga na Dar es Salaam kusindikiza pambano hilo kubwa.
Katika Mchezo huo kutakua na DVD za mafunzo ya mchezo wa ngumi pamoja na kutambua sheria zake mbalimbali zitakazokua zikisambazwa na kocha wa mchezo huo, Rajabu Mhamila 'Super D' kwa ajili ya kuwapa mambondia mbalimbali mbinu za mchezo na mashabiki kujua sheria za masumbwi.
Super D alisema katika DVD hizo kutakuwa na mapambano mengi ambayo yanaweza kutumika kama mafunzo muhimu kwa mabondia, makocha marefa pamoja na mashabiki wa mchezo kujua sheria mbalimbali.
''Kuna mapambano kama ya akina Amir Khan, Manny Pacquiao, Floyd Mayweather, David Haye, Mohamedi Ali pamoja na Mtanzania Roger Mtagwa anaefanya shughuli zake za mchezo huo nchini Marekani.
Pool kambini kwa michuano ya Afrika
Na Hamisi Magendela
Timu ya taifa ya mchezo wa 'Pool Table' inaendelea na maandalizi yake vizuri ya kwa ajili ya kushiriki mashindano ya Afrika yanayonza kutimua vumbi Novemba 22 mwaka huu.
Akizungumza na Jambo Leo Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Chama Cha Pool Table Tanzania (TAPA), Amos Kafwinga, alisema wachezaji wake wako katika hali nzuri na morali kubwa ya mashindano.
"Kwa sasa ndiyo tunashughulikia masuala madogo yaliyosalia ikiwemo hati za kusafiria, ili kila mchezaji akamilishe vigezo vyote vya kuweza kusafiri na kwenda kushiriki bila ya mataizo yoyote," alisema Kafwiga.
Timu hiyo iliingia kambini siku chache zilizopita maeneo ya Tandika 'Davis Corner', na wakiwa katika maandalizi kamambe ya kufanya vizuri katika mashindano yatakayofanyika nchini Malawi.
Wachezaji wanaounda kikosi hicho ni Charles Venance, Omari Akida, Geodfrey Mhando, Mohamed Idd, Antony Thomas, Shamisi Nassoro, Abdallah Hussein pamoja na Felix Athanas.
Ligi ya Wilaya Arusha Novemba 6
Mahmoud Ahmad, Arusha
LIGI soka ngazi ya Taifa Wilaya ya Arusha, inatarajia kuanza awamu ya pili Novemba 6 mwaka huu, ambapo timu 12 kati ya 20 zinatarajiwa kumenyana.
Awali ligi hiyo ilianza kwa kuzishirikisha timu 20 na kugawanywa katika makundi manne, na kila kundi lilitoa timu tatu za mwanzo na timu 8 zilizobaki zilishindwa kufuzu mzunguko wa pili.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Soka Wilaya ya Arusha (ADFA), Zakayo Mjema, alisema katika hatua ya pili kila kundi litatoa mshindi, na timu moja itatoka katika kapu kwa kuangalia uwiano wa makundi na kukamilisha timu nne ili ziweze kucheza fainali ya timu hizo na kupata bingwa wa wilaya.
Alizitaja timu 12 zilizofanikiwa kuingia hatua ya pili ni pamoja na Arusha Meat, Arusha Tarent na Azimio kutoka katika Kundi A, na Kundi B timu zilizofanikiwa kuingia hatua hiyo ni Flamingo, C.I.D.T na Kaloleni.
Alisema Kundi C zilizofanikiwa kuingia hatua hiyo ni pamoja na Olduvai, Parot na United Boys na Kundi D kuna timu za Jamhuri, Njiro Rangers na Boshop Durning.
Mjema aameutaka uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuruhusu Uwanja wa Shekh Amri Abeid kutumika katika hatua hiyo, kwani lengo la chama ni kukuza michezo mkoani Arusha.
Ligi ya Wilaya Arusha Novemba 6
Mahmoud Ahmad, Arusha
LIGI soka ngazi ya Taifa Wilaya ya Arusha, inatarajia kuanza awamu ya pili Novemba 6 mwaka huu, ambapo timu 12 kati ya 20 zinatarajiwa kumenyana.
Awali ligi hiyo ilianza kwa kuzishirikisha timu 20 na kugawanywa katika makundi manne, na kila kundi lilitoa timu tatu za mwanzo na timu 8 zilizobaki zilishindwa kufuzu mzunguko wa pili.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Soka Wilaya ya Arusha (ADFA), Zakayo Mjema, alisema katika hatua ya pili kila kundi litatoa mshindi, na timu moja itatoka katika kapu kwa kuangalia uwiano wa makundi na kukamilisha timu nne ili ziweze kucheza fainali ya timu hizo na kupata bingwa wa wilaya.
Alizitaja timu 12 zilizofanikiwa kuingia hatua ya pili ni pamoja na Arusha Meat, Arusha Tarent na Azimio kutoka katika Kundi A, na Kundi B timu zilizofanikiwa kuingia hatua hiyo ni Flamingo, C.I.D.T na Kaloleni.
Alisema Kundi C zilizofanikiwa kuingia hatua hiyo ni pamoja na Olduvai, Parot na United Boys na Kundi D kuna timu za Jamhuri, Njiro Rangers na Boshop Durning.
Mjema aameutaka uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuruhusu Uwanja wa Shekh Amri Abeid kutumika katika hatua hiyo, kwani lengo la chama ni kukuza michezo mkoani Arusha.





No comments:
Post a Comment