Na Hamisi Magendela
NADIRIKI kusema wakati mwingine sanaa ni kipaji ambacho mwanadamu huzaliwanacho na kama kikiendelezwa, mhusika anaweza kufika mbali na kuitangaza nchi kimataifa.
Wapo wanaoanzia ukubwani na kuwa mahiri katika sanaa, lakini kwa wale wanaonza tangu utotoni wanakuwa na uwezo wa hali ya juu na kufanya makubwa zaidi na ikiwa atasimamiwa vema na kuendelezwa.
Salmin Sindo 'Kiduku' ni mtoto ambaye anaonekana kuwa na kipaji cha hali ya juu katika michezo aliyoshiriki inayooneshwa kupitia luninga ya ITV akiwa na kundi la Jakaya Theatre.
Ni mtoto anaeaminika kuwa anaweza akaja kuwa msanii mzuri na mwenye uwezo mkubwa katika sanaa ya maigizo ikiwa ataendelezwa katika nyanja hiyo ambayo inaweza kumpatia ajira kama ilivyo kwa wengine.
Pia, anaweza kulitangza vema Taifa kutokana kuonekana kivutio wakati wote anapopata nafasi ya kushiriki katika michezo mbalimbali ambayo inamfanya aweze kutambulika kupitia sanaa hiyo ukiwemo ule wa Kovu la Siri.
Katika mchezo wa Kovu la Siri, ambao ulikuwa kwake ni wa kwanza, alimudu vema nafasi yake aliyoshiriki kama mtoto anaelelewa na baba mlevi.
Licha ya utoto wake katika mchezo huo, Kiduku alionekana kumshauri mambo mazuri baba yake ikiwemo kuachana na ulevi ambao ni hatari kwa maisha yake.
Mashabiki mbalimbali waliokuwa wakifuatilia mchezo huo walikuwa wakijiuliza uwezo wa mtoto huyo ulitoka wapi kwa kuwa maneno aliyokuwa akiyatumia yalikuwa na uzito wa kiutuuzima.
Kipaji cha msanii huyo chipukizi kiligunduliwa na Eddy Senzige, ambaye ni mmoja wa viongozi wa kundi hilo, baada ya kumuona nyumbani kwao Kimara Rombo, Dar es Salaam.
Senzige alivutiwa na mtoto huyo baada ya kumuona ana kipaji, ucheshi na utundu, pia wakati wote anaposhiriki michezo ya kitoto na wenzake, hali iliyomsukuma kumuongeza kwenye kundi hilo.
![]() |
Salmin Sindo 'Kiduku' msanii chipukizi mwenye makeke mengi kwenye michezo anayoshiriki |
Anasema mtu anayepangwa naye kucheza anatakiwa kuwa makini kutokana na majibizano yanayokuwepo baina yao kwa wakati huo kwani ana uwezo mkubwa wa ubinifu.
Kaimu Mkurugenzi huyo, anasema siku zote wamekuwa wakimlisha maneno papo kwa papo kutokana na kutoweza kushika maneneo kwa njia ya muongozo (Script), lakini wakati mwingine amekuwa akitoka nje ya muongozo na hutumia busara zaidi kumrudisha katika muongozo.
"Msimamizi anatakiwa kutumia busara na umakini mkubwa kumkatisha pindi anapokosea wakati wa upigaji picha (Shooting), kwa maana huwa ni mwepesi wa kususa.
Anasema ikiwa atakosolewa mara kwa mara hukasirika na anasusa kuendelea na mchakato huo hadi abembelezwe, na ikitokea hivyo inawezekana mchakato huo ukaishia hapo hadi siku nyingine, na hiyo ndiyo changamoto kubwa kwa mtoto huyo.
Msanii huyo ambaye alianza kutembea akiwa na umri wa miaka mitatu anachukizwa na sehemu ambayo mwigizaji anawasilisha ujumbe kwa hadhira kwa njia ya kulia, na ikitokea hivyo, huondoka kabisa katika eneo hilo.
Binafsi, Kiduku anasema huwa anashindwa kuvumilia hali ambayo hujisikia, hasa anapoona watu wazima
![]() |
Salmin Sindo 'Kiduku' akiwa katika pozi |
Chipukizi huyo ambaye alizaliwa Mei 9, 2005 na baada ya miaka miwili mama yake mzazi alifariki dunia, na hadi sasa analelewa na baba akiwa sanajari na mama yake wa kambo.
Licha ya kuendelea kumudu vema sanaa ya maigizo, kwa sasa msanii huyo anasoma darasa kwanza katika Shule St Anne iliyoko Mbezi kwa Msuguri.
Kiduku, tangu alipojiunga na kundi hilo tayari ameshiriki michezo sita ambayo imekuwa ikitamba kwenye luninga na baadhi yake ni Kovu la Siri, Kivuko, Ridhiki, Barafu la Moto na mengineyo.
Msanii huyo anasema lengo lake ni kuwa msanii anayetambulika kwenye tasnia hiyo ambayo itamsaidia kupata matangazo ambayo yatamsaidia kuendesha kumsomesha.
0718594040
Kitale mtukutu, mkali wa vichekesho
Na Hamisi Magendela
SIKU za hivi karibuni, sanaa ya maigizo kwa upande wa vichekesho imekuwa ikijipatia umaarufu mkubwa na kujizolea mashabiki kochokocho.
Inawezekana sababu kubwa ya kujizolea umaarufu huo ni kutokana na ubunifu wa hali ya juu kutoka kwa waigizaji wake, ambao kila kukicha wanabuni mikakati mipya ya kuteka mashabiki.
Kwa sasa, baadhi ya vichekesho hutumika kwenye miito ya simu, hali ambayo inazidi kuwainua na kuwapa umaarufu mkubwa baadhi wasanii ambao wameonesha uwezo mkubwa katika uwajibikaji wao.
Mussa Kitale 'Kitale' ni mmoja wa wasanii wa sanaa ya vichekesho anayefanya vizuri na kujipatia umaarufu mkubwa kutokana na uhodari wake katika kufikisha ujumbe kwa hadhira.
Msanii huyu, licha ya kuwa mchekeshaji, pia ni miongoni wa wachezaji wazuri wa filamu ambaye anaamini siku moja atakuwa msanii bora nchini na kimataifa kutokana na kujituma kwake katika kuboresha kazi zake.
![]() |
Mussa Kitale 'Kitale' msanii anayefanya vyema katika sanaa ya ugizaji uteja |
Katika kundi hilo hakuweza kuwika kama ilivyo sasa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo wakati, kwa maana kila kitu kinakwenda na wakati na wakati wake wa kufanya vizuri umefika.
Msanii huo ambaye wakati anaingia Kaole alipolewa na Mzee Pwagu pamoja na Mzee Kipara ambao sasa ni marehemu wakiwa chini ya Chris Mhenga na kudumu kwa mwaka mmoja kabla ya kutua kwenye kundi la Fukuto Arts Group.
Wakati akiwa katika kundi hilo chini ya kiongozi Tuesday Kihangala 'Mr Chuzi', ndipo alipoanza kuonekana vema na kupata umaarufu kutokana na kuigiza kama mtumiaji aliyeathirika dawa za kulevya 'teja'.
Akiwa katika kundi hilo, Kitale alifanikiwa kushiriki michezo kadhaa ikiwemo ya Ua Jekundu na Jumba la Dhahabu, ambayo ilijizolea umaarufu mkubwa na kuzoa mashabiki lukuki.
"Nikiwa katika kundi la Fukuto nilipata kujifunza mengi nikiwa chini ya Mr Chuzi na kuanza kujulikana kutokana na kuhimili vema nafasi ya kuigiza uteja ilhali situmii kilevi chochote," anasema Kitale.
Msanii huyo aliyezaliwa Desemba 12, 1987 jijini Dar es Salaam, anasema anafakiwa kumudu kuigiza uteja kutokana na kufanya mazoezi ya kutosha na baada ya kufanya utafiti.
Kupitia sanaa, msanii huyu amefanikiwa kuwa na kiwanja eneo la Kimara, ambacho anategemea kuanza ujenzi wakati wowote, pia Kitale alikuwa akimiliki gari, lakini kutokana na sababu mbalimbali aliamua kuliuza.
Kitale, anasema utofauti wake katika sanaa ya maigizo umemfanya kupata umaarufu mkubwa na kusababisha wasichana kumpigia simu mara kadhaa kumtaka kimapenzi.
"Napata shida sana na wasichana kwani wengi wao wanakuwa wakinipigia simu wakionesha wazi kunitaka kimapenzi, lakini niliyenaye ananitosha kwani nimeshazaa naye mtoto mmoja, anaitwa Hemed, ana mwaka mmoja sasa," anasema Kitale.
Anasema katika maisha yake anafikiria kuwa na watoto wanne ambao ndio ana uwezo wa kuwamudu kwa kuwapeleka shule na kuwajengea misingi bora ya maisha.
Mkali huyo wa vichekesho, licha ya kuwa msanii, pia anajishughulisha na biashara ndogo ndogo ambazo zinamsaidia kumuongezea kipato cha kuendesha maisha yake bila matatizo yoyote.
Licha ya kuwa mchekeshaji, Kitale pia ameweza kucheza filamu mbalimbali ikiwemo yake mwenywewe inayoitwa 'More Than A Lion,' ambayo kwa sasa ipo sokoni.
Pia, anafanya muziki wa kizazi kipya na anatarajia kuachia wimbo wakati wowote akianza na video uliokuwa kwenye mahadhi ya Mchiriku unaoitwa' Hili Toto', uliorekodiwa katika studio ya Kwanza ya Mjini Morogoro.
0718 594040
Mwamvita Shaibu:
Mkali kwenye anayewika Five Star
Na Hamisi Magendela
"NAJISIKIA faraja kuimba wimbo uliobeba jina la albamu, naweza kusema ni moja ya mafanikio katika tasnia ya muziki tangu nianze kuingia katika maisha yangu ya muziki."
Hayo ni maneno ya msanii wa muziki wa taarab nchini, Mwamvita Shaibu, alipofanya mahojiano na mwandishi wa makala haya siku chache zilizopita, na leo ikiwa ndiyo siku ya uzinduzi wa albamu hiyo yenye jina la 'Mwenye Hila Habebeki.'
Mwanadada huyo mcheshi ni miongoni mwa wasanii waliomo katika kundi la muziki wa taarab la Five Star, ambao wamekuwa gumzo katika viunga mbalimbali vya jiji la Dar es Salaam na nje ya mipaka ya Tanzania.
Nyota huyu katika nyanja hiyo ya muziki wa taarab alianza kujihusisha na fani hiyo tangu akiwa kidato cha kwanza katika shule ya sekondari ya Makurumla, Dar es Salaam mwaka 1997, iliyokuwa ikitoa elimu ya sekondari ya jioni baada ya masomo ya wanafunzi ya shule ya msingi kuisha na kubadilishwa jina na kuitwa Mwalimu Nyererere.
"Dah! nilianza kujishughulisha na fani hii katika kundi la taarab la Tandale, wakati huo nikiwa mwanafunzi wa shule ya Sekondari Makurumla ya pale Magomeni, Mwembechai, kwa sasa inaitwa Mwalimu Nyerere, ambayo ilikuwa ikitoa masomo ya jioni wakati huo," anasema Mwamvita.
Kutokana na muziki kuwa akilini mwake aliweza kupanga ratiba yake vizuri bila ya kukosa kufanya mazoezi ya kuimba katika kundi la Tandale Modern Theatre, kabla ya kuacha shule akiwa kidato cha tatu baada ya kuegemea zaidi katika muziki.
"Ukweli shule ni kila kitu katika maisha ya mwanadamu, lakini wakati ule muziki ulinizidi na hatimaye nikaangukia huko na hadi sasa naendesha maisha yangu kupitia fani hiyo," anasema nyota huyo.
Mwamvita Shaibu msanii wa muziki wa Taarabu kutoka kundi la Five Star |
Mkali wa kibao kilichobeba jina la albam katika kundi la Five Star cha Mwenye Hila Habebeki, anasema wakati akiwa na kundi la Tandale, aliweza kuimba baadhi ya nyimbo kama vile Hakuna Kulala, Segela na Kiti Cha CCM, ambazo pia ziliweza kufanya vizuri.
Baada ya kazi yake kusikika na wadau mbalimbali wa muziki, mwaka 2003 alihama kundi hilo na kwenda katika kundi la New Zanzibar Stars, wakati huo likiongozwa na Fadhiri Juma.
Kama ilivyokuwa ada ya viongozi mbalimbali pindi anapohama mmoja wa wasanii katika kundi husika, siku zote viongozi wa kundi hujisikia vibaya, ndivyo ilivyokuwa viongozi wa kundi hilo la Tandale Modern Theatre.
"Hali hiyo ilitokea, lakini kama unavyojua pale nilikuwa kama msanii mwanafunzi, hivyo kitendo cha kuitwa katika kundi la New Zanzibar Star, ilikuwa ni sehemu ya kukua katika fani hiyo, japo viongozi wangu hawakudhirika na hilo, lakini wakati ulikuwa umefika wa kuonesha kipaji katika tasnia hiyo," anasema.
Mafanikio hayo kutoka bendi moja kwenda nyingine aliweka wazi kuwa ilikuwa ni sehemu ya mafunzo pamoja na malezi mazuri aliyoyapata kutoka katika kundi la Tandale.
Anasema mafaniko anayoyapata hivi sasa hana budi kuwashukuru viongozi wa Tandale kwa kutengeneza kipaji chake angali akiwa kinda katika sanaa hiyo, ambacho sasa anakitumia kuendesha maisha yake.
Wakati alipokuwa New Zanzibar Star, aliweza kuimba baadhi ya nyimbo ikiwemo Sivyo Nilivyo, Jirani, Nifanye Nini Kwa Waja na nyinginezo ambazo zilifanya vyema kwa wakati huo na kumtangaza zaidi katika medani hiyo.
Pindi alipopata taarifa za kuhitajika alishtuka na kuhisi anahitaji kufanya kazi ya ziada ili kuhakikisha anafanya vyema katika uwanja wa taarab na kupata mafanikio makubwa kupitia muziki huo.
"Nashukuru nilipata mapokezi mazuri na kufanya kazi zangu kwa nafasi, kitu ambacho kilinipa fulsa kubwa ya kujifunza na kuonekana na wadau mbalimbali katika ulimwengu huu wa taarab," anaongeza Mwamvita.
Muimbaji huyo anapenda kuona amani ya wasanii ikiendelea kudumu kila siku na kuvumiliana kwa yote yanatokea katika tasnia hiyo kwani hakuna aliyekuwa mkamilifu chini ya jua.
Alisema baadhi ya wasanii wamekuwa na tabia ya kuwekeana uhasama kutokana na mambo mbalimbali yanayoendelea katika makundi yao, ikiwa baada ya kuimba vibao, wengine wanahisi wanaimbwa wao na kuanza chuki.
Nyimbo zinazoimbwa mara huwa zitokana na matukio mbalimbali yanayojiri katika katika jamii na ndiyo sababu kubwa inayofanya watu kuguswa na wengine kuhisi kuimbwa wao kitu ambacho si kizuri.
Msanii huyo anayewazimia Zuhura Shabani pamoja Hadija Yusuph, anasema anafarijika zaidi kuona nyota hao wakiimba, ambapo anajifunza mambo mengi kupitia kwa hao.
"Ukweli nimejifunza mengi kupitia kwao kwa uimbaji wao, huwa unanikuna kila ninapowasikiliza na ninaamini kutokana na jitihada ninazozifanya nitafikia kiwango chao katika uimbaji," anasema mama huyo wa mtoto mmoja aitwaye Husna.
Mwanamama huyo, aliyezaliwa Machi 3, 1980 jijini Dar es Salaam, anasema mafanikio aliyoyapata kupitia muziki ni pamoja na kufahamika na kufanikiwa kujenga nyumba iliyo maeneo ya Kimara Bonyokwa, ambayo kwa sasa iko katika hatua za mwisho za ujenzi.
Anasema kupata sehemu ya kuweka ubavu ndani ya jiji la Dar es Salaam ni faraja kubwa kwake na kutoa ushauri wa wasanii wenzake kutojisahau pindi wanapopata nafasi kukumbuka kujenga.
Nyota aliyehitimu elimu ya shule ya msingi Mchikichini 1996, wakati huo akitumia jina la Sophia Bakari, anasema malengo yake ya siku za baadae ni kuwa mwalimu wa muziki huo ambao umetawala akili yake.
Pia, anawahamasisha wasanii wenzake kuepuka majungu katika shughuli zao, kitu kitakachofanya kuufikisha mbali muziki huo na kujituma kusaidia kufanikiwa katika muziki huo wa mwambao.
"Tufanye kazi wala tusiogope majungu kwani hiyo ni changomoto katika maisha yoyote yawe kazini au nyumbani, kikubwa ni kujituma zaidi hakika Mwenyezi Mungu ni wetu sote, kinachotakiwa ni kujituma zaidi na mafanikio yapo kwa ajili yetu na dawa ya fitna ni kuzipuuza," anasema.
Anasema, kupuuza fitna na kujituma ndiyo kuliko mfikisha hapo halipo na kuwa na hamu kubwa ya kufanikiwa kupitia muziki huo ambao anamini njia ya mafanikio mengi siku za usoni.
Kwa sasa, nyota huyo amebeba jina la albamu mpya ya Five Star, ambayo leo inafanyiwa uzindizi katika Ukumbi wa Travertine, Dar es Salaam, na kuhahidi kufanya makubwa kutokana na maandalizi mazuri aliyoyafanya wakati wote akiwa na kundi hilo.
ciooo
No comments:
Post a Comment