Mkali wa karate anayesumbu Tanzania
- Ni matunda ya Sensei Chikoko
Na Hamisi Magendela
KARATE ni moja ya mchezo inayokuwa kwa kasi tangu karne ya 19 Japan katika visiwa vya Ryukuyu 'Okinawa' na kusambaa katika nchini mbalimbali ikiwemo Tanzania.
Mchezo huo wa kujiami ulianzishwa na Gichin Funakoshi mwenye uraia wa China, na kuboreshwa katika nchini mbalimbali na kuongezeka mbinu za mchezo huo kulingana na eneo husika.
Ukweli wachezaji wa mchezo huu wamekuwa tofauti sana na wanamichezo mingine kutokana na nidhamu waliyonayo uwanjani na nje ya uwanja wanaonesha utilivu wa hali ya juu.
Mchezo huo umeganyika katika aina tofauti za uchezaji, ambapo kuna aina ya Don Jitsu, hii ni moja ya mtindo unaotumia mikono katika kumkabili adui, wakati aina ya Do Kyohan hutumia zaidi fimbo katika kupambana na kumdhibiti adui.
Pia, kuna aina mbalimbali za uchezaji ambao ni pamoja na Shotocan, Gujuruu na Taekwondo, ambazo ni baadhi tu ya aina ya michezo ya Karate ambayo uchezwa katika nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania.
Katika klabu nyingi za mchezo huo, ni nadra kuwakuta wasichana wakishiriki mchezo japo mchezo haubagui jinsia kwa maana yeyote anaweza kucheza na kuumudu vyema ikiwa atazingatia mazoezi yanayotolewa na wakufunzi.
Rehema Hamad ni miongoni wa wasichana wachache wanaocheza mchezo na kuwa kivutio popote anapokwenda kufanya mazoezi na wengi wakitaka kujua jinsi anavyoweza kuumudu mchezo huo.
Msichana huyo aliyezaliwa Julai 13, 1985 katika Hospitali ya Magunga iliyopo Wilaya ya Korogwe, Tanga, anasema alianza kuupenda mchezo huo angali akiwa mdogo na kulazimika kuwa na ndoto ya kuucheza pindi atakapopata nafasi.
Mkali huyo anasema pindi alipomaliza elimu ya msingi jijini Tanga 2002 katika shule yaKorogwe, alihamia Dar es Salaam na kujiunga katika Dojo ya Leopard iliyopo Kawe.
"Nilipofika Dar es Salaam ndoto yangu ya kucheza karate ilitimia baada ya kuona kuna sehemu ya kufanya mazoezi ndipo nikamfuata kiongozi katika kundi hilo Sensei Philip Chikoko na kumueleza lengo la kutaka kujinga, akaniruhusu," anasema Rehema.
Anasema baada ya kuanza kufanya mazoezi aliweza kufanikiwa kumudu na kucheza mchezo huo vizuri na kuwashangaza watu mbalimbali wakiwemo anaoishi nao karibu na kuonekana tofauti na wasichana wengine.
Msichana huyo anasema sababu za kujiunga katika mchezo huo ni kutokana na ndoto za muda mrefu alizokuwanazo za kuwa miongoni mwa wachezaji mahiri wa karate nchini kwa upande wa akinadada.
"Wazazi hawana tatizo na mimi kuwa mchezaji wa karate kwani nilikuwa na kiu siku nyingi na sasa yametimia na nitahakikisha nafanya vyema na kuonesha kiwango kizuri katika ulingo huo," aneleza.
Mwanadada huyo anaweka wazi kuwa kutokana na kucheza mchezo huo amekuwa mtulivu muda wote na akiepuka ugomvi katika maeneo yote anayokuwepo.
Anasema tangu aingie katika mchezo ameshiriki mashindano mara moja ya kufunga mwaka ya mwaka jana yaliyofanyika katika uwanja wa ndani wa taifa na kufanikiwa kunyakua medali ya dhahabu.
Anasema katika mashindano hayo, aliweza kuwashinda wasichana 10 waliokuwa wakishindana katika mashindano hayo na kumpa chachu ya kufanya vyema katika mchezo huo.
![]() |
Rehema Hamad mkali wa mchezo wa karate |
Kutokana na jitihada alizozionesha katika karate, Rehema hadi sasa ana mkanda wa rangi ya kahawia, na kubakiza mkanda mmoja kufikia mkanda mweusi, ambao ni wa kiwango cha juu katika medani ya mchezo huo.
Katika suala zima la uhusiano, anasema kwa sasa hajaolewa japo ana rafiki wa kiume na ambaye anatarajia kupanga nae maisha na kutarajia kuwa na watoto watatu katika maisha yake.
Pia, anatoa wito kwa wazazi na walezi kuwaruhusu watoto wa kike kujiunga katika mchezo, ambao licha ya kujilinda, pia unasaidia kulinda afya na kuwa mkakamavu wakati wote.
Kiongozi wake katika mchezo huo kutoka katika klabu ya Leopard ya Kawe, Tanganyika Parkers, Dar es Salaam, Sensei Phillip Chikoko, anasema msichana huyo amekuwa mfano kwa akina dada wengi na kuwataka kufuata nyao zake na ndiyo pekee katika klabu yake.
Sensei Chikoko anasema mwanadada huyo ni lulu katika 'Dojo' lake na anajivunia kuwepo kwake na kuahidi kumsaidia kufikia mafanikio ya juu katika fani hiyo.
0718594040
Madina Idd Hussein:
Anayetesa katika gofu bila kocha
Na Asmah Mokiwa
MADINA Idd, ni moja kati ya wachezaji wa timu ya taifa ya gofu (Tanzanite), aliyechangia kwa kisi kikubwa mafanikio ya timu hiyo kuibuka na ubingwa katika mahindano ya wanawake ya Afrika Mashariki na Kati 2011.
Mchezaji huyo ambaye pia ni nahodha wa Tanzanite, mbali na kuchangia mafanikio hayo, pia ni mchango mkubwa kwa wachezaji wenzake pindi wanaposhiriki mashindano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.
Katika mahojiano maalum na Jambo Leo wiki hii, Madina anasema ndoto zake ni kuwa mchezaji wa kimataifa na anayetegemewa na taifa katika mashindano mbalimbali.
“Navutiwa sana na napenda kuwa kama Lee Westwood kwa kucheza, na kila kitu kuhusu yeye, na ndiye aliyenifanya nivutiwe na mchezo huu,” anaeleza Madina.
Lee Westwood ni mchezaji wakimataifa kutoka nchini Japan (PGA), mwenye mafanikio kupitia mchezo wa gofu duniani.
Madina anasema kuwa siri ya yeye kuwa mchezaji mzuri katika gofu ni pamoja na kutumia akili katika uchezaji na kufanya mazoezi mara kwa mara ya mchezo huo, ikiwemo kushiriki katika mashindano mbalimbali nchini.
Nahodha huyo wa timu ya taifa ya wanawake anaeleza historia yake kuwa alianzia katika kazi ya ubebaji wa vifaa vya mchezo huo (Cadian), katika klabu ya Arusha na baadae kujiingiza katika uchezaji.
“Awali nilikuwa si mchezaji wa gofu, na sikuwa nafikiria kuwa nitakuwa mchezaji mzuri wa gofu, lakini baada ya kuingia katika klabu ya Arusha ndio nikaona kuwa gofu ni mchezo mzuri, ndio maana nikajiingiza huko,” anasema.
Anaeleza kuwa mapenzi yake katika mchezo wa gofu yalianza mara baada ya kufanya kazi katika klabu hiyo ya Arusha kuanzia 2001 alipokuwa na umri wa miaka 16.
Alikuwa katika kazi ya ubebaji wa vifaa vya mchezo huo kwa muda wa miaka 6, ambapo mwaka 2006 alianza kucheza mara baada ya kupata ufadhili kutoka kwa watu wa Ujerumani.
Alipata ufadhili huo kutoka kwa wachezaji wa klabu hiyo nchini Ujerumani ambao ni Tonny Shwaller na mkewe Doris Shwaller, baada ya kuona bidii yake katika kazi ya ubebaji wa vifaa walimtaka na yeye awe mchezaji kama wao.
“Nilitumia siku za Jumatatu, ambapo ilikuwa siku ya mapumziko kwangu na kufanya mazoezi kwa kupitia uzoefu niliokuwa nao kwa kutembea na wachezaji wa klabu hiyo pindi walipokuwa wanacheza,” anaendelea kusema Madina.
Baada ya hapo alianza kufanya mazoezi mfululizo ambapo alialikwa katika mashindano mbalimbali nchini ili kuongeza ushindani katika mashindano hayo.
Alianza kucheza mfululizo katika mashindano mbalimbali nchini ambapo baada kuonekana kuwa ni mchezaji mzuri wadau wa mchezo huo walimchagua kuingia katika kikosi cha timu ya taifa.
2009 alicheza katika kikosi cha timu ya taifa kilichokuwa na wachezaji wanne waliokuwa wakishiriki katika mashindano ya Afrika Mashariki na Kati, na Tanzania kuibuka na ushindi kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo yaliofanyika nchini uganda .
Baadaye, alishiriki katika mashindano yalioandaliwa na kiwanda cha sukari mjini Moshi ya (TPC Open), na kuibuka mshindi wa mashindano hayo.
2010, alifanikiwa kushiriki mashindano ya gofu nchini Afrika Kusini ya ‘Sandlam Championship’ yaliyoshirikisha nchi mbalimbali za Afrika ikiwemo Tanzania , ambapo alishiriki na kuwa mmoja kati ya wachezaji walioingia katika hatua ya 50 Bora kati ya wachezaji 151 walioshiriki.
Washiriki hao 50 waliingia katika hatua ya ‘match play flight’ na Madina kuibuka na ushindi wa pili kutoka nchini Tanzania .
Katika mashindano ya All Africa Games ya mwaka jana yaliofanyika nchini Nigeria , Madina alikuwepo katika kikosi cha timu ya taifa na kufanikisha timu hiyo kushika nafasi ya pili kati ya nchi 14 zilizoshiriki mchezo huo katika mashindano hayo.
Katika michezo yote hiyo aliyoshiriki, Madina anasema kuwa moja kati ya mashindano yaliomvutia katika uchezaji na ushindani uliopo ni mashindano ya mwaka huu ya Afrika Mashariki na Kati , yaliyoshirikisha nchi nne na Tanzania kuibuka na ubingwa wake.
“Napenda nilivyoshiriki mashindano ya Afrika Mashariki na Kati ya msimu huu, nilivyoshiriki hadi kufanya timu yangu imepata ushindi.
“Nina mipangilio mingi sana katika maisha yangu, haswa katika mchezo wa gofu, kama nikipata ufadhili wa kutosha nitaenda kusomea zaidi ili niweze kuwa mchezaji wa kimataifa.
“Nikishapata elimu ya kutosha kuhusiana na mchezo huo nitaitumia elimu hiyo kufungua sehemu ya kufundishia wachezaji chipukizi wa gofu ili nao waje kuwa wachezaji wazuri baadaye,”anasema.
Madina Idd Hussein: |
Changamoto anazokutana nazo Madina ni pamoja na kukosa kocha wa kumfundisha na badala yake kufanya mazoezi mwenyewe na kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali anayoshiriki.
Anasema kama Serikali au wadau watapatikana kusaidia kufundisha wachezaji wasiokuwa na makocha, huenda wakanufaika zaidi na vipaji hivyo vilivyosahaulika.
Madina anawataka vijana wenye vipaji vya kucheza mchezo huo wasiogope kujiunga na klabu za gofu kwa kudhani kuwa wachezaji wa gofu ni matajiri sana .
WASIFU WAKE
JINA: Madina Idd Husein
ALIPOZALIWA: Kondoa, Dodoma
ANAPOISHI:Arusha
KLABU ANAYOCHEZEA: Arusha Gymkhana Club
Pia ni mchezaji wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Tanzanite’
No comments:
Post a Comment