VIJIJI VITATU MBINGA VINAVYONUFAIKA NA MAJI YA RUWASA - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Tuesday, December 6, 2022

VIJIJI VITATU MBINGA VINAVYONUFAIKA NA MAJI YA RUWASA

 


Mradi wa maji wa Amanimakoro wilayani Mbinga ambao umegharimu zaidi ya shilingi milionu 448 unaotekelezwa na RUWASA tayari umeanza kuwanufaisha wananchi

MMOJA  wa wanannchi katika kijiji cha Amanimakoro akichota maji katika moja ya vituo vya kuchotea maji

MRADI  wa maji wa kijiji cha Paradiso wilayani Mbinga ambao serikali kupitia  RUWASA imetoa shilingi milioni 249 kutekeleza mradi huo ambao umeanza kuwahudumia wananchi tangu Agosti 2021

Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA nchini Mhandisi Clement Kivegelo akifurahia mradi wa maji Paradiso wilayani Mbinga aliofanya ziara ya kikazi kukagua miradi ya maji mkoani Ruvuma

……………………………

NA MWANDISHI WETU

VIJIJI vitatu vya Amanimakoro,Mkeke na Paradiso katika Halmashauri ya Mbinga mkoani Ruvuma vimeanza kunufaika na miradi  miwili ya maji  inayosimamiwa na RUWASA iliyogharimu zaidi ya shilingi milioni 700.

Meneja RUWASA katika Wilaya ya Mbinga Mhandisi Mashaka Sinkala ameutaja mradi wa maji wa kwanza kuwa ni wa Amanimakro  unatekelezwa  na serikali kwa zaidi ya shilingi milioni 448.

Ameutaja mradi huo kuwa unahudumia vijiji vya  Amanimakoro,Mkeke na kitongoji cha Mkeso katika Kijiji cha Luhagara na kwamba vijiji vyote vina wakazi wapatao 5022 ambao wananufaika na mradi huo.

Hata hivyo amesema mradi huo wa maji ni miongoni mwa  skimu nne ambazo ni Amanimakoro, Lihale, Mkako na Kigonsera zinazosimamiwa na Jumuiya Jumuishi ya watumiaji maji ngazi ya jamii.

“Ili kuweza kukusanya maduhuri kwa ufanisi,Jumuiya inaendelea na uunganishaji wa maji kwa wateja majumbani sanjari na ufungaji wa dira za maji ambapo wateja 75 katika mradi huu tayari wameunganishiwa maji’’,alisema.

Amesema Jumuiya hiyo ni miongoni mwa Jumuiya tano katika Mkoa wa Ruvuma zinazofanya vizuri  katika  ukusanyaji maduhuri ambapo hadi sasa Jumuiya hiyo imeweza kukusanya zaidi ya shilingi milioni 10.

Ameutaja mradi mwingine wa maji kuwa ni unaotekelezwa katika Kijiji cha Paradiso chenye wakazi wapatao 1893 ambapo serikali kupitia RUWASA imetoa zaidi ya shilingi milioni 249 kutekeleza mradi huo ambao umeanza kutoa huduma za maji tangu Agosti 2021.

Mhandisi Sinkala ameutaja mradi huo kuwa ni miongoni mwa skimu za Jumuiya za Raunda, Kindimbajuu,Ntunduwalo,Paradiso na Ndongosi zinazosimamiwa na Jumuiya Jumuishi ya watumaji maji ngazi ya jamii katika kata za Raunda na Namswea.

Amesema Jumuiya hiyo inaendelea na uunganishaji wa maji kwa wateja na kwamba hadi sasa Jumuiya hiyo imeweza kukusanya maduhuri zaidi ya shilingi milioni 17 hadi kufikia Oktoba 2022.

Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA Mhandisi Clement Kivegelo amewapongeza mameja wa RUWASA wilaya ya Mbinga na Mkoa wa Ruvuma kwa kusimamia vizuri miradi ya maji ambayo imeanza kuwahudumia wananchi.

Amesema RUWASA inaunga mkono kwa vitendo kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo kichwani na kwamba Rais amesema hataki kusikia ndani ya uongozi wake mama  anasafiri umbali mrefu kwa ajili ya kutafuta maji.

“Kama kuna jambo ambalo Mheshimiwa Rais ataacha rekodi katika nchi hii ni katika eneo la maji ambayo yamekuwa kero kubwa hasa kwa mama na mtoto tangu nchi hii ipate uhuru’’,alisistiza Mhandisi Kivegelo.

Mbunge wa Jimbo la Mbinga vijijini Mheshimiwa Benaya Kapinga amempongeza Rais Samia kwa kutatua kero ya maji katika wilaya ya Mbinga hasa katika Kata za Amanimakoro na Kijiji cha Paradiso Kata ya Ruanda.

Ametoa rai kwa wananchi waliopokea miradi ya m aji kuendelea kuitunza miradi hiyo ili iwe endelevu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

No comments:

Post a Comment