SAUT WAHAMASISHWA KUHUSU MILIKI UBUNIFU - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Wednesday, May 10, 2023

SAUT WAHAMASISHWA KUHUSU MILIKI UBUNIFU

                 Makamu Mkuu wa Chuo cha Mtakatifu Augustino  (SAUT) cha Jijini  Mwanza, Prof. Costa Mahalu (kulia) akizungumza na Maafisa wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni  ( BRELA) walipomtembelea ofisini kwake kabla ya mafunzo ya Miliki Ubunifu kwa Wahadhiri na Wanafunzi wa chuo hicho tarehe 9 Mei,  2023.
 Prof. Mahalu ameipongeza BRELA kwa kuandaa mafunzo hayo na kufika katika Chuo hicho ambacho  kinafundisha taaluma  mbalimbali ikiwemo Miliki  Ubunifu na Elimu ya Biashara.







NA MWANDISHI WETU

WANAFUNZI na Wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT) wamehamasishwa kuchagua maeneo ya kubobea katika taaluma ya Kisayansi ili waweze   kuandika maandiko mbalimbali ya maombi ya hataza.

Hamasa hizo  zimetolewa na Afisa Usajili kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bw. Stanslaus Kigosi wakati akitoa elimu ya Miliki Ubunifu chuoni hapo tarehe 9 Mei, 2023 jijini Mwanza. 

Bw. Kigosi amesema kwa sasa kuna uhaba wa wataalam wa kuandaa maandiko ya maombi ya Hataza, hivyo   wakibobea katika maeneo hayo watanufaika.

Bw. Kigosi ameshauri pia ni vyema Wanafunzi wa Kada mbalimbali wakaona umuhimu wa kushiriki mafunzo kama haya kwasababu maisha ya binadamu kila siku yanazungukwa na kazi za Miliki Ubunifu ambazo kimsingi ni chanzo cha mapato kwa wabunifu na watumiaji wa kazi za Miliki Ubunifu. 

"Mtu akiwa na uelewa wa Miliki Ubunifu atajua namna bora ya kulinda ubunifu wake na namna bora ya kuingiza ubunifu wake kwenye soko la ndani na nje”, amefafanua Bw. Kigosi.

Naye Afisa Mwandamizi kutoka BRELA Bw. Raphael Mtalima  amesema kuwa SAUT  inafanya tafiti mbalimbali ambazo matokeo yake  yanaweza kufanyiwa mchakato wa kuwa bidhaa au namna za kutengeneza vitu mbalimbali hivyo, wakilinda vumbuzi hizo zitakuwa na manufaa kwa mbunifu, chuo na jamii kwa ujumla.

Ameongeza kwa mifano kuwa  haki za Miliki Ubunifu ikiwemo Hataza na Alama za Biashara na Huduma zimekuwa na  thamani ulimwenguni hivyo Bunifu wanazo  zianzisha au zibuni wazisajili  BRELA ili zilindwe na ziweze kunufaisha na kusaidia jamii.

Aidha ,Msaidizi wa Usajili  wa BRELA Bw. Nasoro Mtavu amesema kuwa Usajili wa Miliki Ubunifu zote zinazosimamiwa na kulindwa na BRELA zinafanyika kwa njia ya mtandao ambao unapatikana katika tovuti ya www.brela.go.tz lengo ikiwa ni kuokoa muda na kupunguza gharama.

Awali akitoa neno la ukaribisho Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Costa Mahalu amewapongeza BRELA kwa kuandaa mafunzo hayo ya Miliki Ubunifu na kufika katika Chuo hicho ambacho  kinafundisha taaluma  mbalimbali ikiwemo ya Miliki  Ubunifu na Elimu ya Biashara

Pia amewataka BRELA kuendelea kufika katika chuo hicho pale wanapopewa mialiko na kutoa mafunzo kuhusu huduma zinazotolewa na BRELA.

Kwa upande wake Dkt. Samwel Mseti , ambaye ni Mhadhiri wa Masomo  ya Biashara, SAUT amewashukuru BRELA kwa mafunzo ya Miliki Ubunifu kwa wanafunzi na watumishi kwani Chuo Kikuu ni taasisi ya kutoa elimu kwa nadharia na vitendo, hivyo ujio wa BRELA unakamilisha dhana ya kutoa elimu kwa vitendo.

No comments:

Post a Comment