Kamishna wa Kazi Msaidizi anayeshughulikia Mahusiano
kazini Bw. Andrew Mwalwisi akitoa elimu kwa umma jijini Dodoma kuhusu
sheria na miongozo ya kazi, Julai 19, 2023.
OFISI ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu
kupitia Idara ya Kazi imewataka waajiri wa sekta binafsi nchini kuzingatia kima
kipya cha chini cha mshahara kilichotangazwa na serikali mwaka huu kwa kuwa ni
takwa la kisheria.
Kima hicho kilitangazwa katika kupitia tangazo la serikali namba
687 na kilianza kutumia Januari Mosi, 2023 na kimewekwa kwenye sekta kuu 13.
Kamishna wa Kazi Msaidizi, Mahusiano kazini wa Ofisi hiyo,
Andrew Mwalwisi ameyasema hayo Julai 19, 2023 alipokuwa akitoa elimu kwa umma
jijini Dodoma kuhusu sheria na miongozo ya kazi.
Amesema kwa sekta ya kilimo ni Sh.140,000, afya
(Sh.195,000), mawasiliano imegawanyika kuna sekta ya huduma za mawasiliano
(Sh.500,000), huduma za utangazaji na vyombo vya habari, posta usafirishaji
vifurushi ni (Sh.225,000) kwa anayeanzia chini kabisa.
“Kazi za majumbani imekuwa changamoto kidogo
ya kutoelewa kwa majumbani hii sekta imegawanyika kwenye makundi manne kuna
wafanyakazi wa kazi za ndani walioajiriwa na wanadiplomasia na wafanyabiashara
wakubwa wanapaswa kulipwa Sh. 250,000, kuna walioajiriwa na Maafisa wenye
stahiki Sh. 200,000, kuna wanaoishi katika kaya ya mwajiri hawa ndo wengi ndo
wengi wanapaswa kulipwa Sh. 120,000 na wanaokwenda na kurudi Sh.60,000,” amesema.
Alibainisha hoteli kubwa za kitalii kima cha chini ni
Sh.300,000, za kati Sh. 180,000 ,migahawa, nyumba za kulala wageni na baa Sh.
150,000, ulinzi binafsi (kwa kampuni kubwa Sh.220,000 na madogo ni Sh.
148,000), sekta ya nishati (kampuni za kimataifa 592,000 na madogo ni Sh.
225,000), Usafirishaji (wa anga Sh. 390,000, utoaji mizigo na usambazaji
Sh.360,000, nchi kavu kwa madereva wao wanapaswa kima cha chini kiwe Sh.
300,000 kwa mwezi.
“Kuna sekta ya ujenzi (daraja la kwanza Sh.
400,000, la pili hadi la nne sh.360,000, la tano hadi la saba Sh. 320,000),
sekta ya madini (uchimbaji na utafutaji madini Sh. 500,000, wenye leseni
za wachimbaji wadogo sh. 300,000, biashara sh.450,000, madalali sh. 250,000),
huduma za shule binafsi ni Sh. 207,000, sekta ya biashara na viwanda
Sh.150,000, taasisi za fedha Sh. 592,000, uvuvi na huduma ya baharini
sh.238,000 na sekta nyinginezo ambazo hazijatajwa kwenye makundi hayo ni Sh.
150,000 kwa mwezi,” amesema.
No comments:
Post a Comment