NA
STEPHANO MANGO, SONGEA
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na uratibu ambaye
pia ni Mbunge wa Jimbo la Peramiho Jenista Joakim Mhagama ameanza ziara ya
kikazi katika Jimbo la Peramiho ya kukagua miradi inayotekelezwa Jimboni
humo,kuzungumza na wananchi, na viongozi mbalimbali wa Chama cha Mapinduzi na
Serikali
Akizungumza katika ziara hiyo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuleta fedha za
miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea.
Waziri Mhagama alisema kwa
niaba ya wananchi wa Jimbo la Peramiho wanaendelea kumshukuru Dkt Samia Suluhu
Hassan kwa kuendelea kukuza uchumi kwa Wananchi hususani wakulima kwa
kuwasongezea huduma za ruzuku karibu na maeneo yao na kwa bei nafuu, hivyo amewataka
wananchi kutumia fursa ya kilimo vizuri ili kukuza uchumi.
“Pamoja kuwa mnajishughulisha
na shughuli za kilimo pia endeleeni kubuni vyanzo vingine vya kuingiza
mapato kwani Serikali yetu inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika
suala la maendeleo ya wananchi imejipanga vizuri ili kuhakikisha wananchi
wanapata maisha bora na salama”, amesisitiza Waziri Mhagama
Katika ziara hiyo Waziri
Mhagama ameweka Jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa madarasa mawili katika
shule ya msingi Muungano , ambapo madarasa hayo yalianza kujengwa kwa nguvu za
wananchi ambapo Halmashauri ilipeleka fedha kiasi cha shilingi milioni 29.6
kutoka mapato ya ndani na milioni 2.5 kutoka mfuko wa Jimbo kwa ajili ya
ukamilishaji.
Aidha katika ziara hiyo amegawa
vifaa tiba mbalimbali katika Zahanati ya Namatuhi vikiwemo viti vya kutembelea
wagonjwa 6 ambapo viti 3 kati ya hivyo wamekabidhiwa wagonjwa, shuka, drip
stand, taulo za kike, blanketi na vyandarua vya kujikinga dhidi ya Malaria kwa
Wazee.
Aidha, Jenista amewataka
Wananchi kuacha tabia za kukata miti ovyo katika maeneo yao na maeneo yaliyo
karibu na vyanzo vya maji kwani huo ni uharibifu wa mazingira unaosababisha
kukosekana kwa maji.
Vilevile Waziri Mhagama
amewaasa vijana kutojishughulisha na shughuli za kilimo cha bangi na matumizi
ya madawa ya kulevya kwani inaleta athari kubwa katika Afya ya akili.
Ziara hiyo imeanza Julai
9, mwaka huu ambapo ameambatana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya
ya Songea Mwalimu Neema Maghembe, Viongozi wa Chama, Madiwani pamoja na
timu ya Wataalamu






No comments:
Post a Comment