DC KASILDA ATOA MWEZI MMOJA KWA HALMASHAURI - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Monday, August 28, 2023

DC KASILDA ATOA MWEZI MMOJA KWA HALMASHAURI


NA MWANDISHI WETU,  SAME


MKUU wa Wilaya ya Same Kasilda Mgeni, ametoa mwezi mmoja kwa uongozi wa halmashauri hiyo kuhamisha gulio linalofanyika Jumatano hadi Jumapili eneo lililotengwa kwa ajili ya Viwanja vya Michezo Maarufu Kwasa-Kwasa.

Ametoa maagizo hayo wakati akizungumza na wafanyabiashara wa Soko hilo ikiwa ni  mwendelezo wa ziara zake kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wananchi wa Wilaya ya Same ambapo amesisitiza uboreshwaji wa miundombinu kuweka mazingira rafiki kwa wafanyabiashara.

Alisema kitendo cha halmashauri kuruhusu eneo la michezo kutumika kama gulio hakikubaliki kwani kinarudisha nyuma jitihada za serikali kukuza michezo.

Mkuu huyo wa wilaya alisema wanamichezo wamekuwa wakilalamika ila hawasikilizwi hivyo anatoa mwezi mmoja kwa halmashauri kupata ufumbuzi wa kero hiyo.

Kwa upande mwingine DC Kasilda ameeleza kutoridhishwa na hali ya Soko Kuu la Mji wa Same kutokana na uchafu uliokithiri, vyoo vinavyotumika kukosa ubora unaohitajika hivyo kuhatarisha usalama wa afya za wafanyabiashara na wanunuzi wanaotumia soko hilo na kuagiza halmashauri kukarabati haraka iwezekanavyo.

Awali wafanyabiashara wa soko hilo wakitoa malalamiko yao wamemweleza mkuu huyo wa wilaya kuwa soko hilo linakabiliwa na ubovu wa miundombinu, kama mashimo makubwa yaliyo ndani ya soko, kukosekana umeme hali inayosababisha kuendesha biashara kwa shida wakitaharisha pia usalama wao.

No comments:

Post a Comment