NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amemtaka Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Injinia Mohammed Besta kukamilisha usanifu wa kina wa Barabara ya Mkata- Kwamsisi ya km36, ifikakapo Desemba 31 mwaka huu.
Akizungumza katika ziara yake ya kukagua athari za mvua za vuli mkoani Tanga leo, Bashungwa amesema fedha za mradi huo zipo tayari hivyo kinchotakiwa kazi ya usanifu ifanyike haraka ili ujenzi uanze mara moja.
"Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameashatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii hivyo kazi ya usanifu ikikamilika ujenzi uaanze haraka," amesisitiza Bashungwa.
Amezungumzia umuhimu wa watendaji wa TANROADS wa ngazi zote kushirikiana na Mamlaka za Serikali ya Mitaa ili kurahisisha ufuatiliaji wa kazi za wakandarasi na kuwezesha kufuatilia haki za watumishi katika miradi ya ujenzi na hivyo kuleta tija katika utekelezaji wake.
Naye Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Injinia Besta amesema wamejipanga kuhakikisha usanifu unakamilika kwa wakati na taratibu za kumpata mkandarasi wa ujenzi huo unakamilika mapema iwezekanavyo.
Katika hatua nyingine Waziri Bashungwa amemuonya vikali Mkandaras China Railway 15 Bureau Group Corporation anaejenga Barabara ya Mkange-Tungamaa-Pangani yenye urefu wa km 120.8 kuhakikisha anaongeza kasi ya ujenzi wa barabara hiyo na Serikali haitavumilia utetezi wowote unaochelewesha ujenzi huo.
"Gharama za ucheleweshwaji wa ujenzi wa barabara ni kubwa kiuchumi kwa maendeleo ya wananchi hivyo Serikali haitavumilia mkandarasi yoyote atakayechelewesha mradi" ameonya, Bashungwa.
"TANROADS naendelea kuwahimiza wakandarasi na wasimamizi wa miradi ambao hawakamilishi kazi kwa wakati wasipewe kazi nyingine" amesema Bashungwa .
Barabara ya Mkange-Tungamaa -Pangani yenye urefu wa Km 120.8 ni sehemu ya barabara kuu ya mwambao wa Afrika Mashariki inayoanzia Malindi-Mombasa -Lungalunga nchini Kenya na Horohoro- Tanga- Pangani hadi Bagamoyo Makurunge yenye jumla ya km 454 ambapo kukamilika kwake kutafungua uchumi wa mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Tanga.
Waziri Bashungwa amesema Barabara ya Pangani-Saadani-Bagamoyo ijengwe kwa kiwango cha kimataifa kwani barabara hiyo inaunganisha nchi za Kenya na Tanzania.
"Namuagiza Mtendaji Mkuu wa TANROADS kuhakikisha kila mradi unakuwa na Meneja mradi na anaekaa katika eneo la mradi wakati wote.
Kwa upande wa Mbunge wa Pangani ambaye pia ni Waziri wa Maji, Juma Aweso amewapongeza TANROADS kwa ushirikiano mkubwa wa kupambana na changamoto zilizokua zinawakumba wananchi katika ujenzi wa barabara.
"Nawapongeza sana TANROADS kwa ushirikiano wenu wa hali na mali mnafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha ujenzi unaendelea," amesema Aweso.








No comments:
Post a Comment