SERIKALI KUENDELEA KULINDA UHURU WA MAWAZO, KUABUDU - DKT. BITEKO - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Sunday, November 19, 2023

SERIKALI KUENDELEA KULINDA UHURU WA MAWAZO, KUABUDU - DKT. BITEKO

                                            ***********************************************

NA MWANDISHI WETU

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema Serikali itaendelea kulinda kwa nguvu na gharama zote uhuru wa wananchi wa kutoa mawazo, imani na uchaguzi katika dini, hivyo itahakikisha kunakuwa na amani na utulivu  ili  uhuru huo wa kuabudu na kutoa mawazo uwepo muda wote.

Dkt.Biteko amesema hayo Novemba 19, 2023 wakati alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Sherehe za kumpongeza Mhasham Askofu Mkuu Mstaafu, Paul Ruzoka na kumpokea rasmi Askofu Mkuu Mpya wa Tabora, Mwadhama Protase Kardinali Rugambwa. Sherehe zilizofanyika katika Jimbo Kuu Kanisa Katoliki Tabora.

"Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan muda wote amekuwa akisisitiza haki kwa wananchi wote, na ili kuishi katika misingi ya utangamano haki lazima itawale. Rais anataka wananchi wasikilizwe; tunaweza kutofautiana katika maoni na mitazamo lakini kamwe tusivunje umoja wa kitaifa, tuwaunganishe watanzania na tupambane kuwaondoa wananchi katika umaskini na kuwaletea nafuu kubwa ya maisha." amesema Dkt.Biteko

Dkt. Biteko amesema kuwa, Mheshimiwa Rais, msisitizo wake ni kupeleka maendeleo kwa wananchi wote bila kuangalia tofauti zao, ikiwemo maji, barabara, umeme, shule na pia lengo lake ni kuendelea kuwaunganisha wananchi ili kuleta umoja nchini.

Vilevile, Dkt. Biteko amesema kuwa, Rais, Dkt.Samia yupo tayari muda wote kushirikiana na taasisi za kidini nchini kuwaletea maendeleo wananchi.

Ameendelea kusema kuwa, Serikali itaendelea kuhubiri haki na maridhiano kama msingi wa amani wa nchi  na pia itaendelea kuhamasisha wananchi kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili kujiletea maendeleo kwani bila kazi hakuna Taifa.

Katika hatua nyingine, Dkt.Biteko amesema kuwa, Rais ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano  kwa Askofu Mkuu Mpya wa Tabora,  Mwadhama Protase Kardinali Rugambwa kama ambavyo amekuwa akitoa ushirikiano kwa mtangulizi wake Mhasham Askofu Mkuu Mstaafu, Paul Ruzoka.

Kwa upande wa Askofu mpya wa Tabora, Mwadhama Protase Kardinali Rugambwa na  Mhasham Askofu Mkuu mstaafu, Paul Ruzoka wameshukuru kwa ushirikiano ambao Serikali imeendelea kuutoa kwao na wameahidi kutoa pia ushirikiano kwa Serikali.

Sherehe hizo zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali  wa Serikali na chama akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dkt. Batilda Burian na Mbunge wa Nzega Vijijini, Hamisi Kigwangala. Pia walihudhuria viongozi mbalimbali wa madhehebu ya dini kutoka ndani na nje ya nchi, na waumini wa Kanisa Katoliki kutoka ndani na nje ya Mkoa wa Tabora.







No comments:

Post a Comment