Akizungumza katika hafla iliyofanyika leo Novemba 12,2023 katika Ukumbi wa Hoteli ya Mout Meru jijini Arusha, Kairuki amesema moja ya lengo kuu la hafla hiyo ni kuitangaza Tanzania kama kivutio cha utalii na pia soko la utalii la kuvutia na la uhakika kwa wageni wa Marekani.
“Serikali ya Tanzania inahimiza uwekezaji katika miundombinu na maendeleo ya masoko ya utalii na hii ni fursa nzuri kwa kampuni za Marekani kuongeza mauzo na kupata maeneo ya kimkakati ya kukuza uwekezaji barani Afrika” Kairuki amesisitiza.
Aidha, Kairuki ametumia fursa hiyo kuyakaribisha kampuni za Marekani kushiriki katika kukuza sekta ya utalii ya Tanzania.
Amefafanua kuwa Sekta ya utalii nchini Tanzania huzalisha zaidi ya dola Bilioni 2.6 katika pato la Taifa pamoja na kutoa ajira zaidi milioni 1.5 kwa wananchi wake.
Kuhusu ongezeko la idadi ya watalii wanaotembelea nchini Tanzania, Kairuki amesema mwaka jana ulikuwa mwaka wa rekodi kwa utalii nchini Tanzania, ambapo zaidi ya wageni milioni moja walikuja kufurahia maeneo ya ikolojia ambapo jumla watalii 100,600 walikuwa ni kutoka Marekani.
Amesema ongezeko la idadi ya watalii linatokana na kuongezeka kwa utangazaji wa Utalii kupitia Filamu ya “Tanzania the Royal Tour” pamoja na matangazo ya television ya CNN ambapo vivutio vya utalii vinaendelea kutangazwa duniani kote.
Katika hatua nyingine, Kairuki amesema Tanzania itakaribisha kikundi cha wachezaji 120 maarufu wa tenisi na wapenda tenisi kutoka Marekani ambao watakuwa kwenye McEnroe Luxury Safari Tour na Mashindano ya Tenisi yatakayofanyika katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti Desemba,2023.










No comments:
Post a Comment