WAANDISHI WA HABARI WAPEWA MAFUNZO MIKATABA YA KIMATAIFA YA UWEKEZAJI - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Monday, November 27, 2023

WAANDISHI WA HABARI WAPEWA MAFUNZO MIKATABA YA KIMATAIFA YA UWEKEZAJI


NA SELEMANI MSUYA, DODOMA

WAANDISHI wa habari kutoka vyombo mbalimbali nchini wamepatiwa mafunzo kuhusu Mikataba ya Kimataifa ya Uwekezaji ambayo imekuwa ikitekezwa kwenye sekta tofauti.

Mafunzo hayo yametolewa jijini Dodoma na Mtandao wa Muungano wa Asasi za Kiraia zinazofanya Uchambuzi wa Sera za Uwekezaji na Biashara Tanzania (TATIC).

Akizungumza na waandishi hao Mkurugenzi  Mtendaji wa TATIC, Olivia Balilo wakati akifungua mafunzo hayo ya siku mbili, ambapo ameweka bayana kuwa kuna ombwe  katika uandishi wa habari za mikataba ya uwekezaji baina ya nchi na nchi, hivyo kupitia mafunzo hayo anaamini kutakuwa na mabadiliko chanya.

Amesema Tanzania ni moja ya nchi ambayo imeingia mikataba ya uwekezaji na nchi nyingine, hivyo TATIC imeamua kutoa mafunzo ili kuwezesha jamii kupata taarifa za uhakika kuhusu eneo hilo.

"Tumeamua kutoa mafunzo haya kwa waandishi wa habari tukiamini ni kundi muhimu katika kutoa taarifa za uwekezaji wa kimataifa mfano Mikataba ya Uwekezaji kati ya nchi mbili, MIUMBI ambayo sisi Tanzania tumeingia au tunatarajia kuingia na nchi nyingine, iwapo nyie mtakuwa na uelewa ni wazi jamii kwa ujumla itapata elimu ya kutosha,"amesema.

Balilo amesema washiriki wa mafunzo hayo watajifunza kuhusu mikataba ya uwekezaji wa kimataifa na uchumi wa kisiasa, mikataba ya uwekezaji na makubaliano, masuala ya sheria na uchumi na mengine.

Mkurugenzi huyo amesema pia mafunzo hayo wametoa kwa watendaji wa Serikali hasa wizara zinahusiana na mikataba hiyo kama mambo ya nje, viwanda na biashara, sheria na katiba na taasisi zingine mtambuka.

Amesema iwapo wadau hao na waandishi watakuwa na taarifa kuhusu mikataba ya uwekezaji ni wazi kuwa kila pande itanufaika na kuondokana na dhana ya pande moja kunyonywa.

Kwa upande wake Mjumbe wa Bodi ya TATIC, Wakili Steven Msechu amesema hadi sasa Tanzania imesaini mikataba 18 BITs(MIUMBI) na nchi mbalimbali ambayo inatekelezwa kwa hatua tofauti.

Wakili Msechu amesema MIUMBI kama ilivyo mikataba mingine ina faida na hasara zake, hivyo ametoa raia kwa nchi kuangalia wapi wanaweza kurekebisha ili nchi zote ziweze kunufaika.

"Sisi Tanzania tumeingia BIT na baadhi ya nchi kama Canada, Finland, Italia, Mauritius, China, Denmark, Switzerland, Uingereza, Sweden, Ujerumani na Uturuki, pia zipo nchi kama Kuwait, Oman, Jordan, Afrika Kusaini, Zimbabwe, Korea nsa Misri," amesema.

Naye mtoa mada Dk Clement Mashamba amesema changamoto anayoiona katika BIT ni wahusika kushindwa kutafuta taarifa kwa kina, hali ambayo inasababisha madhara kwa nchi.

Dk Mashamba amesema iwapo kila anayepata nafasi kushiriki kwenye michakato ataweka uzalendo mbele ni wazi kuwa manufaa yatapatikana.



No comments:

Post a Comment