NEEC YAPIGIWA CHAPUO ZAIDI - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Thursday, February 15, 2024

NEEC YAPIGIWA CHAPUO ZAIDI

Mjumbe mstaafu wa Bodi ya NEEC, Profesa Lucian Msambichaka
NA MWANDISHI WETU

SERIKALI imeshauriwa kuliongezea Baraza la Taifa la Uwezeshaji Kiuchumi (NEEC) fedha ili liweze kuwahudumia Watanzania wengi.

Ushauri huo umetolewa na Mjumbe mstaafu wa Bodi ya NEEC, Profesa Lucian Msambichaka wakati wa hafla ya uzinduzi wa bodi mpya ya saba. 

Prof Msambichaka,  alisema iwapo Serikali itaongeza fedha NEEC itaweza kutekeleza majukumu yake kikamilifu na kunufaisha Watanzania wengi.

“NEEC ni miongoni mwa taasisi muhimu sana katika kuhimili wa uchumi wa taifa na imefanya  kazi kubwa ya kusimamia ndoto za vijana na makundi maalumu hapa nchini.  

Kama serikali itawekeza nguvu kubwa na kuhakikisha  baraza linakuwa  na mfuko imara wa kiuchumi basi taasisi hii itasaidia kuinua uchumi wa mtu mmoja, makundi na taifa kwa ujumla’’alisema Prof. Msambichika.


Alisema  serikali  ikiliongezea uwezo baraza, ikiwa ni pamoja na  kutenga fedha, basi baraza  litachaniga katika kutimiza  ndoto za Rais Samia Suluhu Hassan za  kukuza ushiriki wa Watanzania, hususani makundi maalum, katika shughuli za kiuchumi.

Wajumbe  wapya wa bodi  ni  Profesa Timothy Simalenga, Theobald Sabi, Wakili Cheggy Mziray, CPA Nicodemus Mkama, Brigadia Jenerali  Aloyce Mwanjile, Dk John Mduma na Dk Hamis Mwenyimvua. 

Profesa Msambichaka aliwataka  wajumbe  kufanyakazi kwa umoja ili kufikia malengo ya baraza ya  kukuza na kuchochea ushiriki wa wananchi katika shughuli za kiuchumi.

Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Beng’i Issa, mbali ya kuwapongeza wajumbe wapya kwa kuaminiwa ameahidi kuwa menejimenti ya NEEC itashirikiana na bodi  na wadau wengine na kufanyakazi kwa bidii ili kufikia azma ya serikali ya kukuza ushiriki wa Watanzania kwenye shughuli za kiuchumi.


 Alieleza kuwa uzoefu wa baraza unaonyesha kuwa wanawake wanakimbilia mikopo wanayoichukulia kuwa ni rahisi kuipata pasipo kujua kuwa riba ni kubwa na itawarudisha nyuma kimaendeleo.

“Tumejipanga kikamilifu kuhakikisha tunafikisha huduma za uwezeshaji katika mikoa yote ya Tanzania Bara ikiwa ni pamoja na kuendesha mafunzo ya elimu ya fedha, namna bora ya  kutumia   mifumo iliyoanzishwa na  serikali  sambamba na  kufanya urasimishaji wa biashara za wahudumiwa,” alisema Issa na kuongeza  kuwa baraza linaendelea kuratibu shughuli za wadau  na kusimamia mifuko ya uwezeshaji ambayo sasa ni 72; 62 imo ndani ya serikali na 10 nje ya serikali.

Alisema NEEC imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha maono na matarajio ya serikali ya awamu ya sita c yanafikiwa.


No comments:

Post a Comment