NA MWANDISHI WETU
WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) inaendelea kutoa huduma muhimu kwa wafanyabiashara na wajasiriamali katika Maadhimisho ya Wiki ya Sheria, yanayoendelea katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Huduma zinazotolewa ni pamoja na usajili wa majina ya biashara, usajili wa kampuni, utoaji wa alama za biashara na huduma, utoaji wa leseni za biashara Kundi A, leseni za viwanda, pamoja na ushauri wa kisheria kuhusu shughuli zinazozisimamiwa na BRELA. Huduma hizi zinatolewa papo kwa papo, ikiwa ni fursa muhimu kwa wafanyabiashara wa sekta mbalimbali.
Maadhimisho haya, ambayo yalianza tarehe 25 Januari 2025 na yatamalizika Februari Moshi, 2025, yamejikita katika kutoa fursa kwa wafanyabiashara kuhakikisha kwamba biashara zao zinakidhi vigezo vya kisheria. Wafanyabiashara wanahamasishwa kujitokeza kwa wingi ili kupata huduma hizo za usajili.
Akizungumza kuhusu maonesho haya, Ofisa kutoka BRELA alisema, “Huduma zote zinazotolewa ni za haraka na kwa njia ya mtandao wa Online Registration System (ORS), hivyo wafanyabiashara wanapata huduma papo kwa papo. Hii ni fursa kwa wale ambao bado hawajasajili biashara zao au hawajafanya mabadiliko kwenye taarifa za kampuni zao, kwani huduma hizi zinapatikana bila usumbufu wowote.”
Mbali na kutoa huduma za kisheria na za usajili, BRELA pia inatoa elimu kwa umma kuhusu namna ya kutumia mfumo wa usajili wa mtandao wa ORS, ambao unarahisisha mchakato wa kupata huduma. Hii ni muhimu kwa wajasiriamali na wadau wa biashara ambao wanahitaji kujiunga na mifumo ya kisasa ya usajili.
Maonesho haya pia ni fursa kwa wafanyabiashara kujenga mtandao wa biashara kwa kushirikiana na wadau wengine wa sekta ya biashara.
Wafanyabiashara wanahimizwa kufika kwenye banda la BRELA ili kupata ushauri wa kisheria na kujua namna ya kuhakikisha biashara zao zifuata sheria na taratibu za nchi. Hii ni hatua muhimu kwa wafanyabiashara wa aina zote, kutoka kwa wajasiriamali wa sekta ya biashara ndogo hadi kwa wale wanaoshughulika na viwanda vikubwa.
Kusajili biashara ni hatua muhimu kwa wafanyabiashara wote, na kwakufanya hivyo kunaepusha matatizo ya kisheria yanayoweza kutokea kutokana na ukosefu wa usajili rasmi. “Huduma zote za BRELA zinatolewa kwa haraka, na hii ni nafasi ya kipekee kwa wajasiriamali kuhuisha taarifa za biashara zao au kufungua biashara mpya kwa kufuata taratibu za kisheria,” aliongeza afisa huyo.
No comments:
Post a Comment