NA WAF, KAGERA
NAIBU Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, amesema Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amesajili timu za usimamizi kutoka ndani na nje ya nchi katika kukabiliana na ugonjwa wa Marburg nchini.
Akizungumza leo, Januari 28, 2025, wakati wa ziara yake mkoani Kagera, Dkt. Mollel amesema jitihada za Serikali inazoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye uimarishaji sekta ya afya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali zimesaidia kufanikisha mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
“Tanzania kwa sasa haina mgonjwa mpya wala muhisiwa wa ugonjwa wa Marburg, shukrani zikiwa kwa jitihada za pamoja kati ya Serikali, wataalam wa afya na wadau wa maendeleo,” amesema Dkt. Mollel.
Aidha, amewapongeza watumishi wa sekta ya afya pamoja na wadau kama Shirika la Afya Duniani (WHO), Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC), MDH, USAID, UNICEF na wengine kwa juhudi zao za kuhakikisha ugonjwa huo unadhibitiwa.
“Tanzania imekuwa nchi ya mfano katika mapambano dhidi ya magonjwa ya mlipuko kwa kuhakikisha hayaenei na yanadhibitiwa kwa haraka,” ameongeza Dkt.Mollel.
Ziara ya Dkt. Mollel mkoani Kagera ni sehemu ya mikakati ya Serikali kuhakikisha elimu ya afya na hatua za kujikinga na magonjwa ya mlipuko zinafika kwa wananchi kwa wakati.
No comments:
Post a Comment