DKT BITEKO ASIKITISHWA KUSUASUA UJENZI LAINI YA UMEME TABORA-URAMBO - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Wednesday, March 27, 2024

DKT BITEKO ASIKITISHWA KUSUASUA UJENZI LAINI YA UMEME TABORA-URAMBO


NA MWANDISHI WETU

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amekagua mradi wa ujenzi wa Kituo cha Kupoza umeme cha Uhuru kilichopo wilayani Urambo mkoani Tabora na kueleza kutoridhishwa kwake na kazi ya ujenzi wa laini ya msongo wa  kV 132 kutoka Tabora hadi Urambo ambayo inatekelezwa na kampuni tanzu ya TANESCO (ETDCO). 


Kazi ya ujenzi wa Kituo cha kupoza umeme cha Uhuru imegawanyika katika sehemu mbili ambapo ujenzi wa kituo cha kupoza umeme unafanywa na kampuni ya TBEA kutoka China ambao wamefikia asilimia 84 ya utekelezaji huku kazi ya ujenzi wa laini ya umeme kutoka Tabora hadi Urambo (km 115) ikifanywa na kampuni ya ETDCO ambao wamefikia asilimia 10 tu ya utekelezaji.


Kufuatia hali ya kusuasua kwa ujenzi wa laini hiyo, Dkt. Biteko ameiagiza Bodi ya TANESCO kumwondoa Meneja Mkuu wa ETDCO Muhamed Abdallah ambaye ameonekana kutotoa kipaumbele katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayosimamiwa na Kampuni hiyo.


“Septemba 17, 2023 nilimtuma Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga kuja kukagua mradi huu na aliwapa maelekezo ya kukamilisha mradi, pia nilimtuma aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO, Meja Jenerali Paul  Simuli kuja kukagua mradi huu Desemba 17, 2023 naye alitoa maelekezo ambayo hayajatekelezwa, hatari iliyopo hapa ni kuwa TBEA atakamilisha kazi mapema mwezi Juni lakini umeme bado hautapatikana kwenye kituo kwa sababu laini ya umeme itakuwa haijakamilika.” Amesema Dkt. Biteko


Dkt. Biteko ameongeza kuwa, kutokukamilika kwa wakati kwa laini ya umeme kutoka Tabora hadi Urambo kutapelekea Serikali kumlipa TBEA gharama ya kuwepo eneo la mradi bila kazi ambayo ni asilimia 0.2 ya gharama za mradi na hii ikiwa ni hasara kwa Serikali.


Amesema kuwa,  kampuni ya TBEA na ETDCO zote zililipwa malipo ya awali ya utekelezaji wa kazi kwa asilimia 50 lakini ETDCO anatekeleza kazi kwa kusuasua huku TBEA akifanya kazi kwa wakati.



No comments:

Post a Comment