NA MWANDISHI WETU
KILO 767.2 za dawa za kulevya zimekamatwa katika majiji ya Dar es Salaam na Tanga na Mkoa wa Pwani pamoja watuhumiwa 21.
Dawa hizo na watuhumiwa hao wamekatwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) katika oparesheni maalumu iliyofanyika April 4 hadi 18 mwaka huu kwenye maeneo hayo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Aprili 22, 2024 , Mkurugenzi wa DCEA, Kamishna Kamishna Jenerali, amesema aina ya Dawa za Kulevya zilizokamatwa ni heroin kilo 233.2, methamphetamini kilo 525.67 na skanka kilo 8.33.
"Watuhumiwa 21 wamekamatwa kuhusiana na dawa za kulevya zilizokamatwa, baadhi yao wamefikishwa mahakamani na wengine watafikishwa baada ya taratibu za kisheria kukamilika" amesema Lyimo.
Amezitaja operesheni zilizofanikisha ukamataji wa dawa hizo kuwa ni ilizofanyika jijini Tanga eneo la Mikanjuni Aprili 4, ,2024 ambapo watuhumiwa wawili walikamatwa na gramu 329.412 za heroin, Wailes Temeke mtaa wa Jeshini jijini Dar es Salaam Aprili 8, 2024 na kufanikisha watuhumiwa wawili kukamatwa na kilogramu 1.49 za skanka, Zinga Bagamoyo mkoani Pwani Aprili 10, 2024 walikamata watuhumiwa watatu wakiwa na kilogramu 424.84 za dawa ya kulevya aina ya Methamphetamine.
Pia mtuhumiwa mwingine mmoja alikamatwa na gramu 158.24 za heroin eneo la Kunduchi jijini Dar es Salaam Aprili 10, 2024.
"Aidha Aprili 14, 2024 tulifanya operesheni katika eneo la Bandari jijini Dar es Salaam na tulikamata kilogramu 4.72 za dawa za kulevya aina ya skanka na kuwakamata watuhumiwa watatu kuhusika na dawa hizo.
Aprili 16, 2024 tuliendelea na operesheni jijini Dar es Salaam, katika Kata ya Kunduchi na kukamata kilogramu 232.69 za heroin na kilogramu 100.83 za methamphetamine zilizokuwa zinaingizwa nchini kupitia Bahari ya Hindi.
Watuhumiwa waliokamatwa katika tukio hilo ni tisa" amesema Lyimo.
Pia amesema mtuhumiwa mmoja alikamatwa Aprili 18, 2024 katika eneo la Bandari jijini Dar es Salaam akiwa na kilogramu 2.12 za skanka.
Ameongeza kuwa kwa sasa wasafirishaji wamekuwa wakitumia mbinu mpya katika kuficha dawa hizo haramu na tayari wamezibaini na wataendelea kuzing'amua ili kuwakamata na kudhibiti uingizwaji na utumiaji.
Ameeleza kuwa baadhi ya dawa zilizokamatwa zilikuwa zimefichwa kwa ustadi kwenye vifungashio vilivyoandikwa majina ya kahawa na chai ili kukwepa kukamatwa.
Akiangazia tishio la dawa za kulevya linalokua kwa kasi duniani, Kamishna Lyimo ametoa wito kwa jamii kuungana katika kupambana na janga la dawa za kulevya kwani vijana ni kundi linaloathirika zaidi.
"Vijana ni nguvu kazi ya Taifa letu. Kama wakiendelea kuathiriwa na dawa za kulevya, uchumi na usalama wa nchi vitakuwa hatarini. Ni wajibu wa kila mmoja wetu kupambana na janga hili. Tunawaomba wananchi waendelee kutoa taarifa za watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya ili kulinda taifa letu dhidi ya janga hili kwa kupiga namba yetu ya bure 119” amesema Lyimo.
Kamishna Jenerali Lyimo ametoa shukrani kwa wadau wote wanaoshirikiana na DCEA katika vita dhidi ya dawa za kulevya, hasa vyombo vya ulinzi na usalama na kuahidi kuwa DCEA itaendelea kupambana ili kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi salama na isiyo na dawa za kulevya.
No comments:
Post a Comment