NA MWANDISHI WETU, MBEYA
MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amewataka wananchi kutambua kuwa mafanikio yaliyopo mkoani humo yanatokana na jitihada zinazofanywa na Rais wa Awamu ya Sita, Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye ni zao la Muungano.
Pia ametoa rai hiyo mapema leo Aprili 22, 2024 eneo la Uhindini lilipokuwa soko la zamani wakati wa dua ya kuliombea Taifa ikiwa ni sehemu yamaadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ulioasisiwa na Rais wa Kwanza wa Tanzania Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Hayati Sheikh Abeid Amani Karume.
Amesema kuwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulitokana na ukaribu, ushirikiano wa kijamii na katika harakati za ukombozi dhidi ya mkoloni, uliokuwepo baina ya nchi mbili hizi.
Ameeleza kuwa ni kutokana na Muungano huo umewaunganisha wananchi na kuwa na wigo mpana wa fursa mbalimbali za kijamii, kiuchumi na kisiasa na hatimaye tumeweza kumpata Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ni kiongozi mahiri.
"Matunda ya Muungano ni pamoja na uwepo wa amani, upendo na utulivu ambao umewezesha kuwa na mafanikio mbalimbali katika Mkoa wa Mbeya kama ujenzi wa barabara njia nne, barabara za mitaa, stand ya kisasa ya mabasi ya mkoa, soko la kisasa Soko Matola na maboresho katika hospitali ya Rufaa ya Mbeya na hospitali ya Mkoa na kukamilika kwa ujenzi wa uwanjaa wa ndege wa Songwe Mbeya ambao kwa sasa unafanya kazi kwa saa 24, ambavyo vyote vimefanyika na vinaendelea kufanyika katika kipindi hiki chini ya uongozi wa Rais Samia", amefafanua Homera.
Kutokana na hali hiyo, Homera amewasihi watanzania kuendelea kumpenda, kumlinda na kumtunza Rais Samia ili aendelee kutufanya mambo makubwa katika nchi ya Tanzania.
"Maadhimisho ya miaka 60 yanakwenda sambamba na ufikishaji wa treni ya mwendo kasi hadi jiji la Dodoma ambapo viongozi wa dini na wasanii wamesafiri kwa mara ya kwanza kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma kwa mwendo wa masaa manne, hii ni hatua kubwa sana iliyofikiwa baada ya miaka 60 ya Muungano," ameongeza Mhe.Homera.
Pia amewataka wakazi wa Jiji la Mbeya kusherehekea maadhimisho ya miaka 60 ya muungano kwa kupamba maeneo ya biashara, ofisi na hata majumbani kwa rangi za Taifa na kuwahimiza kuwa ifikapo tarehe 25 Aprili, 2024 wananchi wote wajumuike eneo la Mbalizi katika mkesha wa miaka 60 ya Muungano.
Awali viongozi wa dini ya kiislam na kikristo walianza kwa kiliombea Taifa ili liendelee kuwa na utulivu amani na upendo pamoja na kuwaombea viongozi wa nchi ili waendelee kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
No comments:
Post a Comment