NA MWANDISHI WETU
Wadau Jijini Mbeya wameendelea kuwafariji wahanga wa maporomoko ya tope Itezi Mbeya, ambapo kampuni ya GR City Company limited imetoa kilo 500 za mchele, kilo 150 za unga na mafuta ya kupikia lita 30 huku kwa upande wa machifu mkoa wa mbeya wakitoa unga, mchele na maharage.
Mkurugenzi wa Kampuni ya GR City inayojihusisha na biashara ya hoteli Jijini Mbeya, Machemba Gomano amesema kuwa wameguswa na maafa yaliyotokea hivi karibuni huku akisisitiza wananchi hao walioathirika kutokana na nyumba zao kufunikwa na tope, kuendelea kuwa na subira hasa kwa kipindi hiki kigumu.
Kwa upande wa machifu wakiongozwa na Chifu Rocket Mwanshinga amesema kutokana na maafa hayo hawana budi kuendelea kumuomba mungu kwa pamoja huku wakichangia mahitaji ya chakula kwa wahanga hao.
Naye Diwani wa Kata ya Itezi, Sambwee Shitambala ameendelea kutoa shukrani kwa wadau wanaoendelea kuguswa na maafa yaliyosababisha kaya 16 kupoteza mali zao na kuhifadhiwa katika shule ya jirani na eneo hilo.
Amesema kutokana na misaada inayotolewa na wadau mbalimbali wahanga hao wameshapatiwa magodoro na fedha kwa ajili ya kujikimu kwa kipindi hiki.
Mmoja wa waathirika hao, Ayoub Mwakijaja ameishukuru Serikali kwa kuwathamini na kuonesha nia ya dhati ya kuwasaidia na kuwafariji na kwamba wanapitia kipindi kigumu kutokana na kupoteza mali zao na makazi.
Kaimu mkrugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Annamary Joseph amesema miongoni mwa vifaa na mahitaji yaliyotolewa ni pamoja na vilivyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Kitengo cha Maafa ambao wamepiga kambi katika eneo hilo tangu janga hilo lilipotokea na amewaomba wadua kuendelea kujitokeza kwa wingi kuwafariji wahanga hao.
Wahanga hao kwa sasa wanasubiri uamuzi wa Serikali na taarifa rasmi kutoka kwa wataalamu kuhusu hatma yao.
No comments:
Post a Comment