NA WAF, GEITA
KAMBI ya Madaktari Bingwa wa Rais Samia Suluhu Hassan, iliyokita kambi kwenye Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Geita imefanikiwa kumuondolea uvimbe ujulikao kwa jina la Mayoma mama mmoja ambaye jina linahifadhiwa.
Pia Madaktari Bingwa na Bobezi wamewatahadharisha wananchi dhidi ya imani potofu ikiwepo kulogwa pindi wanapokutwa na matatizo na badala yake waende haraka Hospitalini kuwaona wataalam.
Daktari Bingwa wa kinywa na Meno Anord Christian Jovin, kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga anasema, ndani ya siku tatu za kambi hiyo wamepokea zaidi ya wananchi 23 waliofika kutazama afya za kinywa na meno lakini miongoni mwao wamechelewa kufika kutokana na kusikia maneno ya watu wasio wataalam.
"Amefika mgonjwa (jina tunalihifadhi), tumelazimika kumuondolea Taya moja na kumshauri kupandikiza Taya Bandia, chanzo cha haya yote ni kuchelewa kufika Hospitalini" amesema Dkt. Anord.
Dkt. Anord amesema, wapo baadhi ya wananchi wanao washauri bila utaalam kuwa, pindi uvimbe unapoongezeka ndio dalili yakupona inakaribia, kitu ambacho sio sahihi.
"Tatizo la jino ambalo halijatibiwa kwa muda mrefu linasababisha uvimbe mdomoni na usoni ,tatizo hili linaweza kusababisha mgonjwa kushindwa kupumua (airway obstruction) ambapo inaweza kukatiza uhai wake au maambuki kwenye damu (septicemia) hivyo kuathiri utendaji kazi wa viungo vingine muhimu vya mwili (multiple organ failure)" amesema Dkt. Bingwa Anord.
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa watoto wa Hospitali ya Rufaa ya Geita, Joyce Libonge amesema wamepokea watoto 38, katika kipindi cha siku tatu, lakini ukiuliza kwa kina unabaini wengi wao wamechelewa.
"Amefika mtoto, ambaye utumbo ulikuwa umejisokota, ambaye kimsingi tayari tumemfanyia upasuaji, lakini historia inaonesha tatizo nila muda mrefu na amekuwa akiugulia maumivu, lakini elimu duni ilimsababishia kukaa nao, hivyo uwepo wa kambi hii umekuwa chachu ya kutatua changamoto ya mtoto huyu", amesema Dkt. Libongwe





No comments:
Post a Comment