NA MWANDISHI WETU
BUNDI ameanza kulia katika Chama Cha Allience For Democratic Change (ADC), baada ya aliyekuwa mgombea wa nafasi ya uenyekiti, Doyo Hassan Doyo kupinga uchaguzi,uendeshaji wake na utangazaji wa matokeo akidai mchakato wote umevunja katiba na kanuni za chama hicho.
Doyo ametangaza hayo leo, Julai Mosi, 2024 jijini Dar es Salaam mbele ya waandishi wa habari na akijitangaza kuwa yeye bado ni Katibu Mkuu wa chama hicho kwa kuwa ameweka pingamizi ya matokeo ya uchaguzi uliofanyika Juni 20.
“Napinga mchakato mzima wa uchaguzi kwa sababu kuu tatu za kikatiba na kanuni, moja ni kwamba katiba ilisiginwa kupitia ukurasa wa 42 sura ya 10 inayosema “ Mkutano Mkuu wa Uchaguzi utaongozwa na Mwenyekiti wa muda na mwisho wake utakoma pale mwenyekiti mpya atakapotangwaza na atakabidhiwa kijiti cha kuongoza mkutano mkuu.
“Jambo hilo hilo halikufanyika badala yake Hamadi Rashid, mwenyekiti aliyemaliza muda wake aliongoza mkutano huo mwanzo mwisho huku pia hakukuwa na tangazo la kumpa nafasi hiyo, hivyo katiba na kanuni za chama zilivunjwa kwa makusudi.
“Mimi Doyo ndio muhasisi wa chama hiki na nilishiriki kutunga kanuni na katiba ambazo leo zinavunjwa mbele yangu jambo ambalo siwezi kukubali kupigwa kanzu na tobo nikiangalia, kama katiba na kanuni zinavunjwa mbele yangu, je nikiwa sipo katika chama hiki hali itakuwaje,” alihoji Doyo.
Pia ameongeza kuwa hata Msimamizi wa Uchaguzi naye alilkiuka kanuni na katiba ya uchaguzi wa chama hicho, kwani licha ya mwenyekiti mpya kuchaguliwa, hakumtangaza ili achukue madaraka yake kutoka kwa mwenyekiti wa muda ya kuongoza Mkutano Mkuu.
Amefafanua kuwa mshindi wa nafasi ya uenyekiti alikuja kutangaza mwisho wa mkutano mkuu, jambo ambalo ni kinyume na kanuni za uchaguzi wa chama hicho, iliyo kwenye ukurasa wa nane kifungu C inayomtaka mwenyekiti mpya atangazwe na achukue nafasi ya kuongoza kikao kutoka kwa mwenyekiti wa muda, badala yake Hamadi Rashid aliongoza mwanzo hadi mwisho wa mkutano huo.
Doyo ameongez kuwa rufaa yake tayari ameiwasilisha kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Rufaa ya chama hicho na imesainiwa, pia amesistiza kuwa ana vielelezo vya kutosha vitakavyosaidia kufanikisha kupata haki inayostahiki, ikiwemo video inayoonesha matukio yote tangu kuanza kwa mkutano hadi kumalizika kwake.
Pia aliweka wazi kuwa mkutano huo uligubikwa na harufu ya rushwa kutokana na baadhi ya wanachama kugawiwa fulana za chama hicho ukumbini akidai jambo hilo linaonekana wazi kuwa kama sehemu ya rushwa kwa wapiga kura.
Mwandishi wa habari hii, alimtafuta Hamadi Rashid kwa njia ya simu ya mkononi ili kueleza anachofahamu kuhusu tuhuma zinazomkabili za madai ya kuvunja kanuni na katiba ya chama hicho zinazohusu uchaguzi, simu yake iliita bila kupokelea ingawa jitihada zinaendelea kumtafuta ili aleze kuhusu hilo.
No comments:
Post a Comment