NFRA YAJIVUNIA MAFANIKIO ILIYOYAPATA KIPINDI CHA MIAKA MITATU - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Tuesday, August 20, 2024

NFRA YAJIVUNIA MAFANIKIO ILIYOYAPATA KIPINDI CHA MIAKA MITATU


NA MWANDISHI WETU, DODOMA

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Dkt Andrew Komba amesema  taasisi hiyo imepata mafanikio makubwa  katika kipindi cha miaka mitatu ya serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ikiwemo kuwa na maghala ya kutosha kwa ajili ya kuhifadhi  nafaka zinachonunuliwa kutoka kwa wakulima.


“Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, uwezo wa NFRA ulikuwa kuuza wastani wa tani 50,000 tu za nafaka, lakini baada ya taasisi hiyo kujengewa uwezo tumeweza kufikisha hadi tani 1,750,000 kupitia mauzo ya nafaka yanayofanyika ndani na nje ya nchi,” alisema Dkt Komba.


Akiongea na waandishi wa habari Jijini hapa, Dkt Komba  amesema kuwa mafanikio hayo yanatokana uungwaji mkono mkubwa kutoka  serikalini kupitia Wizara ya Kilimo chini ya Waziri wake Bw Hussein Bashe.


“Hii imetokana na kasi ya ukuaji wa taasisi hiyo ambayo imepata mafanikio makubwa ndani ya kipindi cha miaka mitatu iliyopita. Pia katika kipindi  hicho, NFRA kama taasisi ilikuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 50,000 tu za nafaka,” alisema.


Kwa mujibu wa Dkt Komba,  baadaye uwezo huo uliongezeka hadi kufikia tani 351,000 baada ya utekelezaji wa mradi wa uhifadhi nafaka wa miaka mitatu ulioanza mwaka 2018 na kusimamiwa na Wizara ya Kilimo.


“Baada ya uwekezaji huo kufanyika ikiwemo wa miundombino mbalimbali, uwezo wa uhifadhi wa taasisi  umeongezeka hadi kufikia tani 400,000 mpaka kufikia mwezi Juni mwaka huu. Matarajio ya NFRA ni kuwa na uwezo wa kuhifadhi kati ya tani 700,000 hadi 1,000,000 kufikia Juni mwakani yaani 2025,” alisisitiza.


Dkt Komba alisema NFRA kwa sasa imebadilisha mtazamo kutoka kuwa taasisi ya kuhifadhi nafaka pekee  na kuwa taasisi ya kufanya biashara ya nafaka baada ya kutosheleza hifadhi ya chakula cha kutosha hapa nchini ili kuzidi kujiongezea uwezo.


“Tuna mipango ya kupanua biashara zaidi ya kuuza nafaka katika nchi za jirani kufikia matarajio tuliyonayo,” alisema na kuongeza kuwa


NFRA kama taasisi imewajengea uwezo watendaji wake na kuwapa mafunzo ndani na  nje ya nchi ili kuzidi kuwajengea uwezo katika utendaji wao.


“Taasisi pia imeongeza wigo wa masoko kwa kuwatumia wadau tunaofanya nao kazi  nje ya nchi ili kuongeza uchumi wa nchi kupitia fedha za kigeni na biashara inayofanyika,”alisema Dkt Komba na kuongeza kuwa NFRA imejipanga kuwa mkombozi wa mkulima.


Dkt Komba alibainisha kwamba ndani ya kipindi cha miaka mitatu uwezo wa taasisi yake wa kukopesheka kwa ajili ya uwekezaji umeongezeka kutoka bilioni 50 miaka mitatu iliyopita hadi kufikia bilioni 592, ikionyesha kuwa inaaminika na taasisi za kifedha.



No comments:

Post a Comment