NA MWANDISHI WETU
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Dotto
Biteko, amewataka vijana nchini kushikamana na kudumisha amani iliyopo ili
kuendelea kuwa na taifa lenye utulivu na
kuwafanya watanzania wafurahie maisha.
Kiongozi huyo alibainisha hayo leo Septemba
20, 2024 jijini Dar es Salaam wakati akifungua Kongamano Kitaifa lenye agenda
ya amani na Usalama kwa Vijana litakalofikia tamati Jumapili wiki hii.
Katika kongamano hilo ambalo amemwakilisha
Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Biteko aliwasisitiza vijana kuutumia ujana wao
vizuri ili katika uzee wao wasiwe na majuto kwa maana watashindwa kusahihisha
makosa kutokana na umri kuyoyoma kwani jambo hilo linakiwa kufanywa ujanani.
“Wito wangu kwenu vijana shikamaneni,
shikamaneni shikamaneni!, nimelisema mara tatu shikamaneni kwa ajili ya kulinda
amani ya nchi yetu ili tuwe na Taifa la utulivu na tufurahie maisha yetu.
“Ni vizuri mkakumbuka kuwa hiki ni kipindi cha kujiandaa kuwa Baba bora au Mke mwema ili baadae kuwa na Taifa bora, kwani unapokuwa kijana unaweza kusahihisha makosa lakini unapokuwa mzee inakuwa ngumu na kujikuta ukiangukia kwenye majuto’’ amesema.
Akiwekawazi kuhusu maendeleo ya utandawazi na mapinduzi ya kidijitali ambayo yamekuwa yakitoa fursa lukuki kwa Vijana, Dkt. Biteko amesema “Napenda kuwaasa kwamba matumizi ya teknolojia yakawe na malengo ya kuzalisha na kujitengenezea kipato endelevu.
Kwa
kufanya hivyo kutakuza uchumi na kuonesha tija ya nguvu kazi yetu katika taifa
letu. Aidha, siyo teknolojia hii inavyotumika sasa kama majukwaa ya uhalifu,
uchochezi, udhalilishaji wa kijinsia na uvunjaji wa amani iliyojengwa na vizazi
vya watanzania wengi.
“Natamani baada ya kongamano hili nyie wote mlioudhuria hapa mkawe chachu kwa vijana wenzenu mtakao kutana nao, mkawe dira na walimu bora wa amani,’’amesema Dkt. Biteko.
Pia ameongeza kuwa katika kuhakikisha kunakuwepo na mazingira mazuri ya ushiriki na ushikikishwaji wa vijana katika masuala mbalimbali ya maendeleo Serikali imefanyia maboresho Sera ya zamani Maendeleo ya Vijana na Agosti 12 mwaka huu, Sera Mpya ya Maendeleo ya Vijana ya Mwaka 2007, tolea la mwaka 2024 ilizinduliwa.
Amesema sera hiyo imeeleza nia ya dhati ya Serikali kuhakikisha vijana wanaandaliwa kuwa wazalendo, waadilifu na wanaoshiriki kudumisha amani na usalama wa nchi yetu.
Amefafanua kuwa hiyo yote kutokana na kutambua
umuhimu na nguvu waliyonayo vijana na umuhimu wa ushirikishwaji wao katika
katika kujenga nchi yetu na katika kipindi hiki ambacho nchi ipo katika
mchakato wa kuandaa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 aliwataka vijana kutumia
fursa hiyo ili kuhakikisha wanatoa maoni yao yatakawezesha ushirikishwaji wa
vijana kwenye maendeleo.
Pia katika misingi ya amani na usalama na kuwataka
watumie ubunifu wao kupendekeza mikakati rafiki kwa vijana itakayowawezesha
kushiriki kujenga aina ya Tanzania tuitakayo miaka 25 ijayo.
Amesema takribani asilimia 34.4 ya idadi ya watanzania
wote ni vijana ambao ni sawa na asilimia 56 ya nguvu kazi ya taifa na asilimia
46 ya idadi ya watu wote duniani ni vijana waliochini ya umri wa miaka 25.
‘’Wote mtakuwa mashahidi kinachoendelea duniani kote, amani
imepungua, vifo vimeongezeka, matukio ya uovu yamekithiri na baadhi ya mataifa
hayana amani kwa sababu yana migogoro na mivutano ya kisiasa.
“Ni vyema mkatambua kwamba ninyi vijana wa Tanzania pamoja na wenzenu duniani kote mna jukumu kubwa la kutoa hamasa ya kushiriki katika kujenga na kuilinda amani, na msimruhusu mtu yoyote kuichezea tunu hiyo muhimu kwenye mustakabali wa taifa lolote Duniani.’’ Amesema.
Awali Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, William Lukuvi, wakati akimkaribisha, Waziri Biteko kuzungumza amesema vijana wanatakiwa kuwa waadilifu ili kufikia malengo yao.
Kama mnataka kufikia kama umri wangu au wa Waziri
Biteko ni lazima muwe waadilifu na kujiepusha na vitendo viovu, lazima
mtengeneze uzee wenu utakaokuwa bora sasa na si vinginevyo,” amesema.
Naye Msimamizi Mkuu wa Ofisi ya Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa Tanzania, Shabnam Malick amesema kuwa Shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kufadhili programu mbalimbali kuhusu vijana kwa kuwa vijana wana mchango mkubwa katika kuleta maendeleo nchini.
‘’Tunaamini kuwa amani ni nguzo muhimu ya maendeleo na msingi wa maendeleo endelevu ni lazima tushirikishe vijana katika kufanya maamuzi,’’amesema.
Pia Mratibu wa Kongamano hilo, Joseph Malekelea amesema kuwa kongamano hilo linafanyika kuendana na maadhimisho ya Siku ya Amani Duniani linalofanyika Septemba 21 kila mwaka lilianzishwa mwaka 1981 kwa lengo la kukumbusha watu, mataifa na wadau mbalimbali umuhimu wa kudumisha maadili ya amani na usalama.
“Tanzania tumekuwa tukiadhimisha siku hiyo na kwa ubunifu wetu tukamua kuandaa kongamano hili ili tuweze kuona kwa kina je vijana wetu wanaelewa kuhusiana na amani, je wanashiriki katika kudumisha amani katika nchi yetu, je vijana wetu wanashirikishwa katika suala zima la amani, kipi kifanyike kuhakikisha vijana wanakuwa mstari wa mbele katika kudumisha amani.” amesema.
No comments:
Post a Comment