Na Mwandishi Wetu, Arusha
WATANZANIA wameshauriwa kujenga utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara na kuzingatia kanuni bora zenye usalama wa afya zao.
Hiyo inatokana na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza nchini yakiendelea kuathiri nguvu kazi ya Taifa, kwa kushambulia watu wa rika mbalimbali.
Rai hiyo ilitolewa jana jijini hapa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Norland Global Tanzania, Dk Moses Makalla, akizungumza na wanahabari kuhusu namna bora ya watu kulinda afya zao, ili washiriki vema shughuli za kijamii na kiuchumi.
Alisema kuwa Norland Global ni kampuni inayojihusisha na utafiti, utengenezaji na utoaji tiba kwa magonjwa yasiyoambukiza yenye makao makuu China, huku ikitoa huduma za matibabu duniani kwa kutumia bidhaa za asili zilizofanyiwa utafiti wa kina na kuthibitishwa na taasisi za afya kitaifa na kimataifa.
Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2020, magonjwa hayo yalichangia zaidi ya vifo milioni 41, sawa na asilimia 71 ya vifo duniani, ikilinganishwa na milioni 57 vilivyoripotiwa mwaka 2016 huku nchini, magonjwa hayo yakichangia takribani asilimia 33 ya vifo vyote.
Aidha, takwimu za hivi karibuni za Wizara ya Afya, zinaonesha ongezeko kubwa la magonjwa hayo, ambapo Julai 2022 hadi Machi 2023, magonjwa yasiyoambukiza yalichangia wagonjwa wengi kuhudhuria vituo vya afya ambayo ni shinikizo la juu la damu, wagonjwa 1,456,881 wakiripotiwa sawa na asilimia 49, ikilinganishwa na asilimia 34 kipindi kama hicho mwaka 2021/22.
Kisukari kiliripotiwa kwa wagonjwa 713,057 sawa na asilimia 24, huku magonjwa ya mfumo wa hewa yakihusisha wagonjwa 386,018 sawa na asilimia 13, ikilinganishwa na asilimia 10 katika kipindi kama hicho cha mwaka uliotangulia.
Dk Makalla alisema utafiti wa miaka ya 1986/87 ulionesha mtu mmoja pekee kuwa na kisukari, huku watano wakibainika kuwa na shinikizo la juu la damu, hali inayoonesha ongezeko la magonjwa hayo kwa sasa.
.png)




No comments:
Post a Comment