NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, amewataka wamiliki wa Viwanda na maeneo mengine ya kazi nchini kuzingatia kanuni bora za Usalama na Afya Ili kulinda nguvu kazi inayotumika katika uzalishaji viwandani.
Ametoa agizo hilo alipofanya ziara ya kufuatilia umadhubuti ya mifumo ya usalama na Afya katika kiwanda cha Kusindika samaki cha Omega Fish Limited cha jijini Mwanza ukiwa ni mwendelezo wa ziara zake za kikazi za kutembelea Taasisi na wadau mbalimbali wa sekta ya kazi, Ajira na Mahusiano tangu alipoteuliwa kuiongoza wizara yenye dhamana na masuala ya kazi nchini.
Waziri Sangu amesema ni jukumu la Serikali kuhakikisha kwamba nguvu ya nchi inayotumika kutimiza malengo yake hususani utekelezaji wa Dira ya Taifa mwaka 2050 inalindwa kikamilifu na hivyo ameuelekeza Wakala wa Usalama na Afya Mahali pakazi OSHA kuwa karibu na kushirikiana na wawekezaji katika kusimika mifumo madhubuti ya usalama na Afya Mahali pakazi.
"Kanda ya ziwa inashughuli nyingi za kiuchumi ukiachilia mbali sekta hii ya uvuvi ambayo OSHA mmeifanyia Kazi nzuri ya ukaguzi Kuna sekta nyingi kama vile sekta ya madini ambapo Kuna baadhi ya migodi bubu inayoanzishwa pasipo kufuata taratibu za Usalama na Afya," ameeleza Waziri Sangu na kuongeza;
"Hivyo ninaiagiza OSHA kufanya ukaguzi wa kina kwenye maeneo ya kazi nchini yakiwemo ya sekta ya madini ili kuhakikisha kunakuwa na uzingatiaji wa taratibu zote muhimu za Usalama na Afya jambo ambapo ni muhimu katika kulinda Afya za watu na kuongeza tija katika uzalishaji."
Awali Katibu wa jumuiya ya Viwanda vya Kusindika samaki Onesmo Sule, ambaye alikuwepo katika ziara ya Waziri ameeleza changamoto zinazowakabili wasindikaji wa samaki nchini zikiwemo upungufu wa malighafi unaosababishwa kwa kiwango kikubwa na shughuli za uvuvi haramu hivyo kupelekea Viwanda kuzalisha chini ya uwezo jambo linaloathiri Ajira za watanzania pamoja na kupoteza mapato ya fedha za kigeni.
Aidha changamoto hiyo ilielezwa katika risala ya kiwanda cha Omega Fish Limited iliyosomwa na afisa usimamizi wa Rasilimal wa watu wa kiwanda hicho Zena Marjan Juma ambaye alimwakilisha risala hiyo mbele ya Waziri kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda Hamad Alsaman.
Akiongelea changamoto hizo za wadau Waziri wa kazi,Ajira na Mahusiano amesema serikali imepokea changamoto za wadau wa sekta ya uvuvi kwa uzito mkubwa ambapo ameeleza kuwa changamoto hizo zitashughulikiwa kwa ushirikiano baina yake na wizara ya mifugo na uvuvi.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda ambaye aliambatana na waziri Sangu pamoja na watendaji wengine wa OSHA amesema ziara hiyo ya Waziri imelenga kufuatilia utekelezaji wa Sheria na kanuni za Usalama na Afya Mahali pakazi katika kiwanda hicho kwa mujibu wa miongozo ya OSHA.
"Ziara hii ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu yetu ya kila siku ya kufanya ukaguzi wa mifumo ya usalama na Afya katika maeneo mbalimbali ya kazi na kimsingi tumeridhishwa na namna kiwanda hili kinavyotekeleza miongozo ambayo tumekuwa tukiwapatia mara kwa mara," ameeleza kiongozi huyo mkuu wa OSHA.
Kiwanda cha Omega Fish Limited ni miongoni mwa Viwanda 64 vya Kusindika samaki nchini ambacho kinasindika samaki aina ya sangara na kuuza katika nchini mbalimbali za Ulaya na bara la Asia
Kwa mujibu wa takwimu za wizara ya mifugo na uvuvi ni sekta muhimu katika maendeleo ya uchumi wa Taifa. Katika mwaka2023 sekta ya uvuvi ilichangia asilimia 1.7 kwenye Pato la Taifa ( GDP) na kukua kwa asilimia 1.4. Aidha sekta hii inatoa Ajira kwa watanzania takribani milioni 6 zikiwemo Ajira za moja kwa moja kwa wavuvi wapatao 201661 na wakuzaji viumbe majira 49084 katika mnyororo wa thamani.







No comments:
Post a Comment