NA HAMISI MAGENDELA
BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wamesaini makubaliano ya kushirikiana katika kubadilishana taarifa kupitia mifumo ya Tehama kwa lengo la kurahisisha utendaji kazi kwa taasisi hizo kama ambavyo Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ameelekeza.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt Bill Kiwia akizungumza na waandishi wa Habari wakati hafla ya kubadilishana hati za makubaliano leo, Septemba 13, 2024 jijini Dar es Salaam, amesema kwamba baada ya hatua hiyo kufanyika kitakachofuata ni vikao vya mkakati kwaajili ya kuhimalisha mchakato wa ukusanyaji madeni kutoka kwa wanufaika wenye kipato.
“Haya tunayotekeleza hapa ni maelekezo ya Rais wetu Dkt Samia ya kutaka taasisi zote ziwe zinasoma mifumo ili kupunguza muda wa kufuata nyaraka kutoka ofisi moja kwenda nyingine na hadi kufikia Desemba mwaka huu, HESLB tutakuwa tumekamilisha,” amesema.
Pia Dkt Kiwia amesema kuwa jukumu la taasisi yake ni kukusanya mikopo kutoka katika taasisi mbalimbali ambako kuna wanufaika ambao baadhi yao ni wadaiwa, hivyo kushirikiana na TRA kuna faida kubwa katika kufikia malengo.
Aidha Dkt. Kiwia amebainisha kuwa TRA, wanajukumu la kuwatambua walipa kodi katika sekta mbalimbili nchini, hivyo ni vizuri kushirikiana nao kimkakati ili kufanikisha kuwafikia wanufaika wa mikopo popote walipo.
Pia amesema wao kama Bodi ya Mikopo, wanatoa wito kwa wanufaika wa mikopo wenye kipato kufanya jitihada za kuirejesha ili iwanufaishe wengine na kupitia mifumo huo wa kusomana kwa taasisi za Serikali watalifikia kundi kubwa ambao hawajalipa mikopo yao kwa wale wenye kipato.
Vilevile amebainisha kuwa kushirikana na TRA katika kubadilishana taarifa kutawezesha kuinua maendeleo ya nchi hivyo ni jambo la kujivunia kufikia hatua inayotakiwa ya kuunganisha mifumo ya Tehama na taasisi hiyo muhimu nchini.
Naye Kamishna Mkuu wa TRA, Mwenda amesema kwamba wao wanataarifa nyingi watakazobadilishana na HESLB ya kwanza wataanza na taarifa za watumishi wao ambao wana madeni hiyo watahakikisha wanarejesha kwa lengo la kutoa fursa kwa wahitaji wengine kunufaika.
Ifahamike kwamba mafanikio yatakayopatikana ni matunda ya walipa kodi wan chi hii, hivyo ni vizuri wanufaika walipe kwa hiari ili watoto wao wasome vizuri kupitia mikopo watakayopata.
Pia amesema kuwa wana kundi kubwa la wananchi wanaoshughulika na uchumi zaidi ya mil 2 na wanatoa wito kwa wanufaika wote kurejesha mikopo kama inavyotakiwa na kuahidi kutekeleza yote yaliyomo katika mkataba ambao wamesaini.
HESLB Septemba 11, mwaka huu ilibadilishana hati na taasisi tatu ambazo tayari mifumo ya Tehama imeungana nazo ikiwemo Vitambulisho Vya Taifa (NIDA) Wakala wa Usajili ,Ufilisi na Udhamini( RITA) na Taasisi za uchakataji wa taarifa za waombaji mikopo kwenye Taasisi za Fedha (CREDIT INFO,) lengo likiwa kurahisisha utendaji kazi hususan wa kufutilia wanufaika wenye kipato ambao bado hawajalipa, mikopo yao.
No comments:
Post a Comment