NA MWANDISHI WETU
WAKATI mchakato wa uandikishaji majina ya wapiga kura kwenye daftari la mkazi likiendelea, wakuu wa wilaya na wakurugenzi jijini Mwanza,wameagizwa kusimamia sheria Ili wasiharibu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwishoni kwa Novemba 2024.
Agizo hilo limetolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, wakati akikagua vituo vya uandikishaji majina ya wapiga kura, jijini humo.
Mtanda alisema wasimamizi wa uchaguzi wanapaswa kuhakikisha unakuwa huru na wa haki ili kuenzi maono ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ya kuimarisha demokrasia.
"Wito wangu kwa wakuu wa wilaya na wakurugenzi wote kusimamia daftari hili kwa uhakika lakini pia kwa kufuata sheria, kanunu na taratibu za uchaguzi," alisema Mtanda
Mtanda alisema "Rais wetu ni muumini wa demokrasia na demokrasia ni mchakato unaanza kwenye uandikishaji, upigaji kura, kuhesabu kura na utangazaji matokeo."
Mtanda alisema Mwanza imejipanga kikamilifu kusimamia zoezi la uandikishaji wapiga kura ambapo hadi sasa asilimia 63 ya wakazi wa Mwanza wamejiandikisha.
Alisema lengo la Mwanza ni kuhakikisha wananchi wote wanajiandikisha.
"Mawakala wa vyama vyote wapo na chama chochote kinachotaka kuweka wakala kiweke hakuna anayezuiliwa na wataendelea na shughuli zao kama kawaida," alisema Mtanda.





No comments:
Post a Comment