JINSI AMDT INAVYOSAIDIA KILIMO CHA UMWAGILIAJI KWA JAMII YA KIMASAI - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Sunday, October 20, 2024

JINSI AMDT INAVYOSAIDIA KILIMO CHA UMWAGILIAJI KWA JAMII YA KIMASAI

 

   (Picha kwa hisan ya mtandao)

NA MIKE MANDE, SIMANJIRO

KWA muda mrefu sasa jamii ya kabila la Kimaasai nchini Tanzania limekuwa likijishughulisha na ufugaji wa ng’ombe, mbuzi na wanyama wengine wafugwao kama moja ya shughuli za asili na kujinufaisha kiafya na  kiuchumi kutokana na mazao yanayotoka na mifugo hiyo.

 

Hata hivyo mabadiliko  ya tabia nchi ambayo yamesababisha ukame na mvua kidogo katika maeneo kadhaa ya nchi, inayosababisha baadhi ya jamii ya Kimasai wilayani Simanjiro, mkoani Manyara kuanza kujihusisha na  kilimo cha mboga mboga kwa njia ya umwagiliaji kama sehemu ya kukabiliana na ukame na kujiongezea kipato.

 

Mmoja  wa wakulima hao na ambaye amepata mafanikio makubwa, ni Mathayo Olonyoki, mkazi wa kijiji  cha Kirung’rung’ Kata ya Oldonyongijabe, wilayani Simanjiro ambaye ameanzisha kilimo mazao ya mbegu mbegu kwa kutumia umwagilaiji wa matone katika shamba lake la hekari tatu.

 

Olonyoki ambaye pia ni mfugaji anasema kuwa aliamua kuanza kujishughulisha na kilimo hususan cha umwagiliaji baada ya kijiji anachoishi kupata mvua hafifu iliyosababisha mifugo mingi kufa kutokana na ukame unaosababisha kukauka kwa majani ya malisho.

 

Anasema kuwa baada ya kupata mafunzo kutoka Shirika la Beula Seed Co. & Sons Ltd, alianza kujishughulisha na kilimo katika mazao yanayohimili ukame.

 

“Nilianza na kulima katika ukubwa wa eneo la heka tatu la mfano na kupanda zao la maharagwe, mbaazi na choroko ili kuweza kuipatia familia yangu chakula chenye protini na kuachana kutegemea ufugaji tu,” anasema Olonyoki.

 

Katika mradi huo ambao unafadhiliwa na Feed for the future, chini ya mradi Mama wa CIMMYT unaochechemuliwa na Taasisi ya Kukuza na Kuendeleza Mifuko ya  Masoko nchini (AMDT), imemuwezasha Olonyoki, kuendeleza kilimo hicho baada ya kupatiwa ufadhili wa miundo mbinu ya umwagiliaji.

 

Delta Shila, Mratibu wa Tathmini na Ufuatiliaji wa Matokeo wa AMDT anasema, Taasisi hiyo ilianza kuwasaidia wakulima wilayani Simanjiro katika kata za Oldonyongijabe na Mererani ili kukabiliana na ukame na kuifanya jamii ya wafugaji kuanza kujipata kipato kipya badala ya kutegemea mifugo ambayo imeathiriwa na ukame.

 

Shila, anasema AMDT kwa sasa inaendesha mradi wa umwagiliaji katika mikoa ya Manyara, Arusha, Dodoma, Singida, Lindi, Mtwara, Songwe, Ruvuma, Njombe, Tabora, Rukwa na Dar es Salaam ili kupunguza athari  za ukame kwa wakulima wadogo wadogo.

 

“Mradi huu unaendeshwa na AMDT umemsadia Olonyoki na wanakijiji wenzake kupata mazao mengi katika eneo dogo na kuweza kulima mazao kibiashara,” anasema Shila.

 

AMDT ni taasisi ambayo imedhamiria kukuza huduma za soko la mazao kwa wakulima wadogo ili kuongeza kipato chao na ajira kwa akina mama wasiojiweza kiuchumi na vijana kwa kulenga kuinua maisha yao.

No comments:

Post a Comment