(Picha kwa hisani ya mtandao)
NA MIKE MANDE
MTANDAO wa kikundi cha wakulima wa kijiji cha Mkoka, wilayani Kongwa mkoani Dodoma wameanza kufaidika na mradi wa kilimo cha umwagiliaji mashamba unaofadhiliwa na Taasisi ya Kukuza ba Kuendeleza Mifuko ya Masoko nchini (AMDT).
Mtandao huo wenye vikundi 23 vya wakulima vyenye wakulima waliosajiliwa 585 kilimo cha umwagiliaji kimewawezesha kuzalisha mbegu bora wakati wa kiangazi kwa kuvuna tani 5 za mbegu.
Oziniel Benego, Mratibu wa Mtandao huo amesema kuwa wamefanikiwa kuuza jumla ya tani za ujazo 4.5 na kujipatia jumla ya Shilingi milioni 11.4 na kukipatia faida kikundi hicho.
Benego amesema kuwa wameweza kukabiliana na ukame kutokana na kukauka kwa mto uliokaribu na kijiji hicho baada ya kupata msaada kutoka Taasisi ya Kilimo na Maendeleo ya Masoko Tanzania (AMDT) kwa kuwachimbia kisima chenye urefu wa mita 150 chenye uwezo wa kutoa lita 16,000 kwa saa.
Kwa mujibu wa Benego AMDT pia imewawezesha kuwapatia mafunzo ya juu ya uzalishaji mbegu bora ambapo kumewezesha kupatikana kirahisi kwa mbegu hizo kwa wakulima na kwa bei nafuu.
Jumla ya wakulima 600 katika mikoa ya Kilimanjaro, Dodoma, Arusha na Manyara wanashiriki katika mradi wa uendelezaji na uzalishaji wa mazao ya jamii ya kunde ili kuweza kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuongeza matumizi ya teknolojia katika kilimo nchini.
Mradi huo wa AMDT unasaidia kuongeza uelewa wa matumizi ya mbegu bora zinazohimili ukame na mbinu za kurutubisha afya ya udongo ili wazalishe kwa tija.





No comments:
Post a Comment