NA MWANDISHI WETU, MWANGA
HARAMBEE iliyoongozwa na Katibu Mkuu wa Baraza za Waislam Tanzania (BAKWATA) Alhaj Nuhu Mruma Desemba 30,2024 kwa ajili ya ujenzi wa Msikiti wa Maroro Mikuyuni imefanikiwa kupatikana zaidi ya shilingi milioni 33 ya ahadi ya fedha na mifuko ya saruji zaidi ya 450.
Alhaj Mruma aliongoza harambee hiyo katika Viwanja vya Familia ya Kashengena vilivyopo kijiji cha Mikuyuni wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro baada ya kuweka jiwe la msingi la msikiti huo mpya wa kisasa ambao unatakiwa kugharimu shilingi milioni 700 hadi kukamilika kwake na kuswalisha waislam 300 kwa wakati mmoja.
Katika zoezi hiloa uwekaji wa jiwe la msingi na harambee hiyo Alhaj Mruma aliambatana na Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Shaban Simba, Kadhi wa Mkoa wa Kilimanjaro Hussein Chifupa, makatibu wa mikoa wa BAKWATA na wengine.
Mruma alitoa pongezi kwa waislam wa Maroro Mikuyuni kwa uamuzi wao wa kuamua kujenga msikiti wa kisasa ambao unatarajiwa kuwa na ghorofa nne pindi ukikamilika na kugharimu shilingi milioni 700.
Alhaj Mruma aliwataka waislam wa Maroro Mikuyuni kuhakikisha msikiti huo unaongeza umoja, ushirikiano na mshikamano kati yao na sio kuwagawa.
Mruma alisema BAKWATA wapo tayari kushirikiana na waislamu ambao wanaweka maslahi ya umma mbele na sio maslahi binafsi.
"Naomba nichukue fursa hii kwa kuwapongeza waislam wa Maroro Mikuyuni kwa uamuzi huu wa kujenga msikiti mpya, Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania Dkt Abubakary Zubeir anasisitiza ushirikiano," alisema.
Mruma alisema katika kuonesha kuwa wanaunga mkono ujenzi huo BAKWATA taifa watachagia sh milioni 2.5 kwa ajili ya ujenzi wa msikiti huu wa kisasa," alisema.
Aidha, Alhaj Mruma alisema pamoja na BAKWATA pia amewasiliana na wadau mbalimbali wa serikali na binafsi ambao wamemuahidi zaidi ya Sh milioni 10.
Kiongozi huyo alitoa wito kwa waislam wote nchini kubwa makini na watu ambao wanatumia kisingizio cha dini kuibua mifarakano, huku akisisitiza kuwa BAKWATA makao makuu hawatavumilia.
Kwa upande wake Sheikh wa Mkoa wa Arusha, Shaban Simba aliwataka waislam kuisoma dini yao vizuri, ili kuhakikisha wanailewa hali ambayo itaondoa tafsiri hasi pale wanapotoa tafsiri.
"Mnachofanya waislam wa Maroro Mikuyuni kinaonesha namna BAKWATA ilivyo na mifumo sahihi ya kusimamia dini yetu ya Kiislamu, ila napenda kutumia nafasi hii kuwaomba tusome quruan na hadhithi zake na kuelewa vizuri ili kuepuka tafsiri potofu ambayo imekuwa ikitumiwa na baadhi yetu kupotosha," alisema.
Akisoma taarifa ya ujenzi wa msikiti huo, Katibu wa Kamati ya Ujenzi , Yahaya Kambagha alisema msikiti huo wa kisasa unatarajiwa kugharimu Sh milioni 700 pindi ukikamilika wote.
Kambagha alisema katika awamu ya kwanza ya ujenzi wa msikiti huo wanarajia kujenga ghorofa moja ambayo itagharimu sh milioni 400.
"Ramani yetu ni kujenga msikiti wa ghorofa nne, ila kwa sasa tunaanza na ghorofa moja ambapo kutakuwa na sehemu ya kuswalia, vyoo, ofisi, stoo, sehemu ya kuhifadhia na kuosha maiti ambapo sh milioni 400 itatumika," alisema.
Mjumbe wa Kamati ya Msikiti, Alhaj Ashrafal Mruma alisema ujenzi wa msikiti huo wa kisasa unaenda kufungua fursa kwa vijana wa eneo hilo kwa kuweza kusoma madrasa ambapo wataongezewa uelewa kuhusu dini yao.
Alisema mikakati yao ni kuhakikisha wanajenga chuo cha ufundi ili kutoa elimu kwa vijana wa Kitanzania.
Kwa upande wake Fundi Mkuu wa ujenzi huo, Salehe Abdallah alisema msikiti huo unajengwa kwa viwango vyenye ubora na matarajio yao iwapo fedha zitapatikana utakamilika ndani ya muda mfupi.
No comments:
Post a Comment