NA MWANDISHI WETU, KATAVI
HALMASHAURI ya Wilaya ya Mlele imepokea gawio la Shillingi Millioni 210 kutokana na shughuli za uwindaji wa kitalii zinazosimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA wilayani humo.
Gawio hilo ni asilimia 25 ya fedha zitokanazo na faida inayopatikana kutokana na shughuli za uwindaji wa kitalii ambapo asilimia 40 ya fedha hizo huelekezwa katika shughuli za uhifadhi na asilimia 60 kuelekezwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Akizungumza na waandishi wa habari Desemba 14, 2024 wilayani humo Mkurugenzi wa H/W ya Mlele, Sigilinda Modest Mdemu amesema halmashauri yake imenufaika na fedha za gawio kiasi cha shilingi Millioni 210 kutoka TAWA ambazo zimetumika katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa zahanati katika kijiji cha songambele iliyotumia takribani shillingi millioni 150.
Vilevile amesema fedha hizo zimewasaidia kutengeneza madawati kwenye shule za msingi na sekondari, kujenga ofisi za vijiji pia zimesaidia kutoa mafunzo ya usimamizi na uhifadhi wa Maliasili Kwa wataalamu wa Sekta ya Maliasili katika wilaya hiyo.
"Kwa kipindi cha miaka miwili yaani kwa Mwaka wa fedha 2022/23 Halmashauri yetu ilipokea kiasi cha shillingi millioni 210 fedha ambazo ni gawio kutoka TAWA kama sehemu ya uchangiaji wa shughuli za maendeleo ya jamii Kwa vijiji vinavyozungukwa na Hifadhi " amesema Bi Sigilinda Mdemu
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Alhaj Majid Mwanga amesema wananchi wa wilaya hiyo wamekuwa wakifaidika na uwepo wa TAWA kupitia fedha za mapato ya utalii ambapo hupata gawio la dola 5,000 zinazotolewa na wawekezaji Kwa vijiji vinavyozunguka Vitalu vya uwindaji wa kitalii ambazo huzitumia katika ukamilishaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Naye Ofisa Habari wa TAWA, Beatus Maganja ametoa wito kwa Halmashauri zote nchini zinazopokea fedha zitokanazo na shughuli za uwindaji wa kitalii kuzitumia fedha hizo Kwa malengo yaliyokusudiwa ili wananchi waweze kuona faida za rasilimali wanyamapori zinazohifadhiwa nchini.
"Ni muhimu sana fedha hizo zitumike ipasavyo Kwa ajili ya miradi ya maendeleo ili wananchi waone faida ya hizi rasilimali " amesisitiza Maganja
Katika hatua nyingine Ofiisa Ujirani Mwema wa Pori la Akiba Rukwa, Christopher Mlimbila ameomba ushirikiano kutoka Kwa wananchi wa Wilaya ya Mlele katika kulinda na kuhifadhi rasilimali wanyamapori na kutokomeza ujangili huku akitoa wito Kwa wananchi wanaofanya shughuli za kibinadamu katika maeneo ya Hifadhi kuacha mara moja ili uhifadhi uweze kusonga mbele.
Naye Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Kaulolo wilayani humo, Hussein Mwita amesema Kijiji chake kipo tayari kushirikiana na TAWA kikamilifu Kwasababu Kijiji hicho kimeona manufaa ya Taasisi hiyo katika nyanja mbalimbali ikiwemo ujenzi wa ofisi ya kijiji ambayo amesema ujenzi wake ungechukua miaka mingi bila kukamilika kama TAWA isingehusika kutoa fedha hizo zinazotokana na shughuli za uwindaji wa kitalii.
No comments:
Post a Comment