NA MWANDISHI WETU, MWANZA
WAKALA wa Usajili, Ufilisi na Udhani nchini (RITA), umeitaka Bodi mpya ya Wadhamini wa Msikiti wa Ijumaa jijini Mwanza, kujiepusha na ubadhirifu wa mali za msikiti sambamba na kuimarisha mshikamano wa waumini, pamoja na kutolipiza visasi kwa bodi ya wadhamini ya msikiti huo iliyovunjwa awali.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya ofisi kwa bodi mpya ya msikiti wa Ijumaa Jijini hapa, Kabidhi Wasii Mkuu na Ofisa Mtendaji Mkuu wa (RITA), Bw Frank Kanyusi alisema uteuzi wa bodi hiyo mpya umejili baada ya kuwepo kwa mgogoro uliodumu kwa zaidi ya miaka 30, baada ya kufanyika usajili wa mabadiliko ya katiba mnamo mwaka 1990.
“Sababu za migogoro hiyo, ni kutotambulika mabadiliko ya Katiba ya mwaka 1993 yaliyowasilishwa kwa Msajili Mkuu mwaka 1997, kutoelewana wajumbe wa bodi ya wadhamini iliyokuwepo, matumizi mabaya ya mali, fedha na kukosekana kwa uwazi katika Taasisi,” alisema Kanyusi.
Alisema Tarehe 2 mwezi Februari mwaka huu, RITA iliunda kamati ya uchunguzi ambayo ilifanya kazi kwa kipindi cha mwezi mmoja na kukabidhi ripoti iliyoonyesha kuna ubadhirifu wa fedha takribani shilingi bilioni moja ya kitanzania.
“Baada ya tuhuma zilizokuwa zikiikabili bodi iliyopita niliunda kamati ya uchunguzi iliyowasilisha taarifa kwa mamlaka za uchunguzi (TAKUKURU) ambapo mpaka sasa kazi imeshaanza kufanyika, na baadhi ya wajumbe wa bodi iliyopita wameshahojiwa, na hivi punde TAKUKURU itakamilisha kazi yake na wataka bainika katika ubadhirifu huo taratibu za kisheria zitafuatwa ili kila mmoja apate stahiki kwa mujibu wa sheria.” alieleza Kanyusi.
Kanyusi alitoa rai kwa wajumbe wa bodi mpya ya udhamini kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kama sheria inavyotaka, alisisitiza kuwa wao sio wamiliki wa mali bali ni wasimamizi wa mali kwa niaba ya wanachama hivyo wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria.
Aidha, Kabidhi Wasii Mkuu huyo amewashukuru na kuwapongeza waumini wa msikiti huo kwa ustaarabu na utulivu mkubwa waliouonyesha kwa kipindi chote cha kamati ya uongozi wa mpito.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti Bodi Mpya ya Wadhamini ya Msikiti wa Ijumaa. Bw Sherally Hussein mbali ya kuipongeza RITA kwa usimamizi mzuri alisema wakati umefika wa kuunganisha nguvu kwa waislamu wote wa msikiti huo ili kusimamia malengo yaliyo kusudiwa kuanzishwa kwa taasisi hiyo.
“Kwa sasa tuna imani kwani ile mivutano ilitugawa kwa makundi tofauti tofauti, ni wakati sahihi sasa makundi yote kuungana ili taasisi yetu iweze kutoe mchango stahiki kwa waumini wote na taifa kwa ujumla wake,” alisema Hussein.
Ofisi ya Kabidhi Wasii Mkuu nchini (RITA) imeahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa bodi mpya ya wadhamini katika uongozi ili iweze kutimiza majukumu yake kikamilifu kwa maslahi mapana ya waumini ya jumuiya ya kiislam mkoa wa Mwanza
No comments:
Post a Comment