N
A MWANDISHI WETU PWANI
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, (TAKUKURU)
mkoani Pwani inatarajia kukamilisha utafiti mdogo wa kubaini vyanzo vya vitendo
vya rushwa vinavyohusisha baadhi ya askari wa Usalama Barabarani na wataikabidhi
kwa Jeshi la Polisi ili kutoa suluhisho ya changamoto hiyo.
Hayo yamewekwa wazi leo mkoani Pwani, Januari
20, 2025 na Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Pwani, Christopher Mzava wakati
akizungumza na waandishi wa habari na kuongeza kuwa utafiti huo upo katika
hatua za mwisho kukamilika.
“Sisi kama Takukuru wakati mwingine tunafanya
uchunguzi, kama utafiti kutaka kuangalia tatizo lina ukubwa gani na hatua za
kuchukua, hivyo katika kipindi cha kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka na kabla
tulifanya utafiti mdogo kuhakikisha tunapata taarifa sahihi za usalama
barabarani.
“Na sasa tupo katika hatua ya kukamilisha na
tutaipeleka kwa wenzetu Jeshi la Polisi kwa lengo la kuangalia wapi mapungufu
yalipo na nani anajihusisha na vitendo vya rushwa, kwani siku zote rushwa haizuiwi
na mtu mmoja, inatakiwa uwepo wa ushirikiano wa taasisi mbalimbali na ndiyo hali
inayoweza kufanikisha mapambano dhidi ya rushwa,” amesema.
Amesema utafiti huo utawasaidia wao Takukuru
na Jeshi la Polisi kufanikisha kudhibiti vitendo vya rushwa vinavyolalamikiwa na
wananchi hasa wanaotumia vyombo vya usafiri ingawa inafahamika kuwa rushwa ni
siri kati ya mtu na mtu na inawezekana wakati mwingine baadhi ya wenye vyombo nao
wakawa chanzo kwa kushawishi.
“Pia hata baadhi ya watu wetu ambao si
waadilifu nao wanaweza kuwa vishawishi katika vitendo vya rushwa hivyo
vitendo vya rushwa vipo na sio kwamba havipo kwa sababu ni vitu ambavyo vinalalamikiwa.
“Mfano juzi kuna baadhi ambao wameonekana
kupitia picha za video kama ambayo wengi mmeona na tayari hatua zimechukuliwa,”
amesema.
Ameongeza kuwa awali kulikuwa na ushirikiano kati
ya Polisi, Takukuru na Wadau uliokuwa unaitwa (UTATU) na lengo lilikuwa ni
kuhakikisha vitendo vya rushwa barabarani vinatoweka.
Amesema kuwa kulikuwa na App iliyokuwa
inatumika na wadau mbalimbali kurekodi vitendo vya rushwa vikiwa
vinaendelea na baadaye kutuma bila kujulikana kwenda kwenye taasisi husika na
kuchakatwa na hatua kuchukuliwa.
Kamanda Mzava ameongeza kuwa kwa sasa App hiyo
inaonekana kama kulegalega na wao kama Takukuru wanawajibu wa kuhakikisha vitendo
vya rushwa vinakoma na kuiweka nchi salama kutokana na kwamba Tanzania bila ya
vitendo vya rushwa inawezekana.
Mwisho
No comments:
Post a Comment